Tanzia: Askofu Paschal William Kikoti amefariki dunia
Kwa masikitiko , tunatoa habari za kifo cha Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki
la Mpanda, Mkoani Katavi Tanzania , Mhashamu Askofu Paschal William Kikoti, aliyefariki
dunia siku ya Jumanne kwa ugonjwa wa shinikizo la damu , akiwa katika hospitali ya
Rufaa ya Bugando jijini Mwanza. Padre Patrick Kasomo, Vika wa Askofu Jimbo
la Mpanda, alitangaza msiba huo Jumanne mbele ya mamia ya waumini walikusanyika katika
Kanisa Kuu la Mpanda baada ya kupata taarifa hizo. Kwa mujibu wa Padre
Kasomo, Askofu Kikoti alipatwa na shinikizo la damu Jumapili iliyopita majira ya asubuhi
wakati akioga na kuanguka chini ghafla na kupoteza fahamu. Na Mapadre na Watawa waliofika
nyumbani kwake baada ya Ibada ya Misa ya kwanza ya majira ya saa mbili na nusu za
asubuhi, walimkuta katika hali hiyo ya kutojitambua. Na mara walitoa
taarifa kwa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), ambalo lilitafuta usafiri wa ndege
na kumsafirisha hadi hospitali ya Rufaa Bugando Mwanza , ambako alianza kupatiwa matibabu
hadi alipofariki siku ya Jumanne. Marehemu Askofu Kikoti , alizaliwa parokiani
Nyabula , mkoani Iringa mwaka 1957 na kupewa daraja la Upadre June 29 , 1988 mkoani
Iringa. Aliteuliwa kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo la Mpanda na Papa Yohane
Paulo 11 0ctoba 2000, na kusimikwa January 24, 2001. Marehemu Askofu Kikoti
atazikwa siku ya Jumamosi, Mosi Septemba 2012, katika Kanisa Kuu la Mpanda. Tunamwombea
pumuziko la amani peponi.