Mashindano ya Michezo ya XXX ya Olympic 2012: London kunawaka moto!
Kuanzia tarehe 27 Julai hadi tarehe 12 Agosti 2012, Jijini London, viwanja vitakuwa
vinatimuka vumbi katika mashindano ya thelathini ya michezo ya Olympic, tukio linalopaswa
kuonesha tunu msingi za maisha ya kijamii, kiutu na mshikamano wa dhati kati ya watu
wa mataifa.
Michezo ya Olympic kwa mara ya kwanza ilifanyika kunako Mwaka
776 Kabla ya Kristo, huko mjini Olympia, nchini Ugiriki. Haya yalikuwa ni mashindano
kwa ajili ya wanamichezo mahalia tu na wala hayakuwa na umaarufu wowote kimataifa.
Lakini kadiri muda ulivyokuwa unazidi kuyoyoma, michezo mingi zaidi iliendelea kuongezwa
katika mashindano haya, kiasi kwamba, hata muda wa mashindano yenyewe ukaongezeka
maradufu.
Kipindi chote cha mashindano ya Olympic, vita na misigano yote ya
kisiasa na kijamii ilisitishwa ili kutoa fursa kwa wananchi kufurahia michezo nchini
Ugiriki. Kumbe tangu mwanzo, tunu ya amani imekuwa ni kati ya mambo yanayotiliwa mkazo
wakati wa michezo ya Olympic.
Michezo hii ilianza kupata umaarufu wa pekee
mara baada ya utawala wa Kirumi kuanza kushika hatamu za uongozi nchini Ugiriki. Hapa
Ukristo ukatambuliwa rasmi kwamba, ndiyo dini iliyokuwa inaongoza kwenye utawala wa
Kirumi. Wakati wote huu, michezo hii ilionekana kuwa na sura ya kipagani zaidi na
wala hakuna masuala ya kidini yaliyogusiwa wakati huo.
Kunako mwaka 393 wakati
wa michezo ya Olympic huko Thesalonike, kulitokea maafa makubwa yaliyopelekea Mfalme
Theodor wa kwanza kusitisha michezo hiyo! Hapa kukawa ni mwanzo wa kuyumba na kuchechemea
kwa historia ya michezo ya Olympic iliyokuwa imedumu kwa takribani Karne mia moja
Kabla ya Kristo! Hapa si haba!
Mwaka 1894 Bwana Pierre de Coubertin akajitosa
kuhamasisha tena michezo hii miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa kwa kuanzisha mashindano
ya michezo mbali mbali, ikiongozwa na kauli mbiu iliyojulikana kwa lugha ya Kilatini
kuwa ni "Citius, Altius, Fortius" yaani, Kasi, hapa Waswahili wangesema "Mchomoko",
Lenga juu zaidi na kwa nguvu".
Mashindano ya Olympic yamefanyika Barani Ulaya
mara 18, Amerika ya Kusini mara 6, Barani Asia mara 4, Oceania mashindano haya yamefanyika
mara 2. Kwa bahati mbaya kabisa, Mashindano ya Olympic hayajawahi kufanyika hata mara
moja Barani Afrika, tangu kuumbwa kwa ulimwengu!
Mashindano ya Olympic yameendelea
kuboreka mwaka hadi mwaka. Lakini pia yamekuwa yakikabiliana na changamoto mbali mbali
zikiwemo za ulinzi na usalama wa wanamichezo na watazamaji wanaohudhuria katika mashindano
haya. Hii ni dhamana nyeti sana kwa wenyeji wa mashindano haya na kwa Jumuiya ya Kimataifa
katika ujumla wake. Ndiyo maana kuna hatua kali sana za nidhamu zinachukuliwa ili
kuwa na ulinzi makini zaidi hasa kutokana na kuongezeka kwa vitendo vya kigaidi sehemu
mbali mbali za dunia.
Mashindano haya yamekuwa wakati mwingine yakitumiwa
na wanasiasa kama Jukwaa la kupenyeza sera na agenda zao za siri kuhusiana na masuala
ya kisiasa na kibaguzi. Kutokana na baadhi ya wanamichezo kuanza kuonesha tabia ya
ubaguzi wa rangi kwa baadhi ya wanamichezo kutoka Afrika, hatua za nidhamu zimeaanza
kuchukuliwa kwa baadhi ya watu hao kufungiwa na kutoruhusiwa kushiriki katika michezo,
kwani michezo hii ya kimataifa inalenga zaidi kudumisha umoja na mshikamano wa kidugu
miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa.
Baadhi ya wafanyabiashara haramu ya dawa
za kulevya wamekuwa wanataka kutumia mwanya wa michezo hii ya kimataifa kwa ajili
ya kueneza biashara haramu ya matumizi ya dawa za kulevya, matukio yanayowahusisha
wanamichezo wenyewe, kiasi cha kukiuka malengo na kanuni za michezo.
Kashfa
hizi zimekuwa ni aibu kwa wanamichezo na nchi wanamotoka pale inapobainika kwamba,
ushindi walioupata ni kutokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Michezo hii
imeongeza pia kasi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo unaowatumbukiza
wanawake na wasichana katika utumwa na utalii wa ngono.
Mama Kanisa anaona
kwamba, matukio kama haya ya michezo ya Olympic ni mahali muafaka pa kuendeleza mchakato
wa Uinjilishaji Mpya. Ndiyo maana mikakati ya maisha ya kiroho kwa ajili ya wanamichezo
na mashabiki wao inapewa kipaumbele cha pekee, kwa kutambua kwamba, mwanadamu ameumbwa
mwili na roho!
Wakati wa sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili iliyopita, Baba
Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alitumia fursa hii kuwatakia matashi mema waandaaji,
wanamichezo na watazamaji, katika mashindano haya ya kimataifa, ili yawe ni fursa
ya kukoleza udugu, amani na upatanisho sehemu mbali mbali za dunia.