Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limepokea kwa moyo wa furaha na shukrani kuu
habar iza uteuzi wa Askofu Protas Rugambwa aliyekuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma,
kuwa Katibu mkuu msaidizi Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na Rais wa Mashirika
ya Kimissionari ya Kipapa pamoja na kumpandisha hadhi kuwa ni Askofu mkuu.
Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania linasema hizi ni dalili za kukua na kukomaa kwa Kanisa
la Tanzania, tayari kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo,
yaani Kanisa katika ngazi ya kiulimwengu. Wanamshukuru Baba Mtakatifu Benedikto wa
kumi na sita, kwa kutoa heshima hii kubwa kwa Kanisa la Tanzania.
Itakumbukwa
kwamba, Askofu mkuu Protas Rugambwa alizaliwa kunako tarehe 31 Mei 1960, Bunena, Jimbo
Katoliki la Bukoba. Alipata majiundo yake ya Kipadre kutoka katika Seminari ndogo
za Katoke iliyoko Rulenge-Ngara na Itaga, Jimbo kuu la Tabora. Kwa masomo ya Falsafa
alipelekwa Seminari kuu ya Kibosho iliyoko Jimbo Katoliki la Moshi na Masomo ya Taalimungu
aliyapatia Seminari kuu ya Mtakatifu Karoli Lwanga, maarufu kama Segerea.
Baada
ya masomo na majiundo yake ya Kipadre, alipadrishwa kunako tarehe 2 Septemba 1990,
Jimbo kuu la Dar es Salaam wakati wa Hija ya Kichungaji ya Baba Mtakatifu Yohane Paulo
wa Pili nchini Tanzania. Yeye alikuwa ni kwa ajili ya Jimbo Katoliki Rulenge kwa wakati
huo. Baada ya Upadrisho alifanya utume Parokiani, Seminari Ndogo ya Katoke, Mwenyekiti
wa Idara la Liturjia Jimbo Katoliki Rulenge na Mhudumu wa shughuli za kiroho Hospitali
ya Biharamulo.
Kuanzia mwaka 1994 hadi 1999 alipelekwa mjini Roma kwa masomo
kwa masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano na kujipatia Shahada ya
Uzalimivu katika shughuli za kichungaji. Baada ya kurudi Jimboni mwake Rulenge, alipangiwa
kuwa Mwalimu na Mkurugenzi wa miito na Mkurugenzi wa shughuli za Kichungaji; Makamu
Askofu.
Kunako mwaka 2002 hadi 2008 aliombwa kwenda kusaidia kutoa huduma
za kichungaji kwenye Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, utume ambao aliufanya
kwa ufanisi mkubwa. Kunako tarehe 18 Januari 2008, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita, akamteuwa kuwa ni Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma, Tanzania na kuwekwa wakfu
hapo tarehe 13 Aprili 2008.
Baada ya Askofu Protas Rugambwa kuwafundisha, kuwaongoza
na kuwatakatifuza Watu wa Mungu Jimbo Katoliki Kigoma, tarehe 16 Juni 2012, Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita, akamteua kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa
la Uinjilishaji wa watu na Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa.