2012-03-14 07:50:30

Benedikto XVI: dhana ya maisha mintarafu jamii za Kiafrika


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, nakukaribisha tena kwa furaha kabisa tuendelee na uchambuzi wetu wa Hati Dhamana ya Afrika: Africae Munus. Juma lililopita tulizungumzia juu ya vijana na watoto. RealAudioMP3
Tulichambua mambo mengi mintarafu wao ni nani na nafasi yao katika jamii, wajibu wa jamii kwa makundi hayo; na nini Kanisa linafundisha na kutenda juu ya vijana na watoto. Leo Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anatuongoza katika kutafakari kwa kina kuhusu mtazamo wa Kiafrika juu ya maisha.
Maisha kwa mtazamo wa Kiafrika ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu. Maisha yanajumuisha viumbe vyote vilivyo hai na visivyo hai. Ni muunganiko wa walio wazima na waliotangulia mbele ya haki, wanaozungumza na wasiozungumza, waliozaliwa na ambao bado hawajazaliwa, wanaofikiri na wasiofikiri. Kimsingi tamaduni za Kiafrika zinatoa nafasi na heshima kubwa kwa uhai. Kuna imani kubwa kwamba maumbile ya kiulimwengu kama yalivyo, yapo ili kutunza, kulinda na kurutubisha uhai.
Vizazi vilivyopo havina budi kuheshimu vizazi vilivyo tangulia na vijavyo ndio maana kuna miungu na mababu ambao wameabudiwa na kuheshimwa tangu mwanzo; na nyakati za shida huelekezewa maombi ya msaada na jamii husika kama waombezi na waangalizi wa jamii. Urithi huu, anasema Baba Mtakatifu ni nafasi nzuri kwa familia ya Mungu Barani Afrika kuelewa ujumbe wa Kristo, kuthamini fumbo la Kanisa na kuendelea kuthamini maisha katika mtazamo wa Kikristo.
Mababa wa Sinodi katika uchambuzi wao kuhusu kutunza na kuthamini uhai barani Afrika, walizingatia kwa makini jitihada mbali mbali zinazofanywa na jumuiya ya Kimataifa. Hata hivyo waligundua utata kwa baadhi ya jitihada hizo hususan juu ya majina yake na maana yake, ambazo kwa namna fulani zilionekana kupingana na mafundisho na maadili ya Kikristo. Hata hivyo wao hawakusita kutoa mwelekeo sahihi juu ya maisha kadiri ya mafundisho ya Kikristo. Walilaani kwa namna ya pekee matumizi ya njia za kisasa za mpango wa uzazi na kupaaza sauti dhidi ya utoaji mimba.
Baba Mtakatifu alisisitiza kwamba wako watu, makundi, taasisi na hata mataifa ambayo yanapinga msimamo wa Kanisa dhidi ya njia za kisasa za mpango wa uzazi. Lakini Kanisa lisiogope makundi, taasisi na hata mataifa haya, bali lazima lisimamie ukweli daima ili kuhifadhi thamani ya maisha na hadhi ya mwanadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Muumba wake. Amewataka Wanafamilia ya Mungu kuwepo duniani lakini wasijihusishe na mambo ya dunia hii.
Aidha Baba Mtakatifu anaendelea kubainisha mambo ambayo yanaendelea kutishia na kudhoofisha maisha Barani Afrika, ambayo ni pamoja na umaskini, magonjwa na ujinga. Mambo haya yanawatatiza sana watu wa Bara la Afrika, amabapo wengi wao wanaishia katika matatizo na majanga makubwa kama njaa, vita vya wenyewe kwa wenyewe, biashara ya ukahaba, UKIMWI, Kifua kikuu, Malaria, matumizi harem ya dawa za kulevya, utoaji mimba, ubakaji, na imani potofu zinapolekea mauaji ya vikongwe, watu wenye ulemavu wa ngozi, biashara haramu ya viungo vya binadamu na dhuluma nyingine za Kijamii.
Analitaka Kanisa kufanya tafakari ya kina kuhusu hali ya Bara la Afrika na kubuni mbinu mkakati ili kusaidia kutatua na kurudisha nafuu ya maisha kwa watu wa Bara hili. Amezialika taasisi za Kanisa Barani Afrika kuvalia njuga swala la Elimu ambayo anaamini yaweza kuwa ufunguo kwa matatizo mengi. Elimu hii ilenge kumjenga Mwafrika, akatambue barabara mazingira yake hivi kwamba kwa elimu hii aweze kubuni njia za kujijengea maisha pale alipo na kwa rasilmali zinazopatikana karibu naye.
Hii itasaidia kuondokana na fikra potofu kwamba maendeleo ya Afrika lazima yatoke nje ya Afrika. Elimu hii imsaidie kujenga fikra bora juu ya maisha binafsi, mtu mmoja mmoja aweze kutumia mwanga huu kuishi maisha yanayolingana na wakati dunia ilipofikia.
Sanjari na hilo anaialika Jumuiya ya Kimataifa, taasisi na mataifa yenye nguvu kuzingatia na kutenda katika kweli kwani kila mtu akimtazama mwingine kwa viwango anavyojitazama mweneywe vitendo vya kibinafsi vinaweza kukomeshwa. Misaada inyotolewa kwa Bara hili itolewe kwa moyo wa upendo na ilenge miradi ya kumnufaisha kwanza Mwafrika na sio kujenga mirija ya kulinyonya zaidi bara hili. Yaangaliwe maeneo ambayo mwenyeji akielekezwa anaweza kwa msaada kidogo kunyanyua maisha yake na wanajumuiya wenzake.
Hadi hapo tumefikia mwisho wa tafakari yetu kwa siku ya leo. Nakutakia heri na baraka toka kwa Mweneyezi Mungu na mfungo mwema wa kwarema. Ni mimi mtayarishaji na msimulizi wako Padre George wa Bodyo.








All the contents on this site are copyrighted ©.