Kwaresima kiwe ni kipindi kwa watawa kukuza na kudumisha moyo wa upendo na matendo
ya huruma
Kardinali Joào Braz de Avis, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa
na Kazi za Kitume anawakumbusha watawa kwamba, kipindi cha Kwaresima ni mwaliko kwao
wa kukuza na kudumisha moyo wa upendo na matendo ya huruma, hususan kwa watu wanaosukumizwa
pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha.
Hii ni njia muafaka ambayo
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anawaalika waamini na watu wenye mapenzi
mema kuitumia katika kipindi hiki cha Kwaresima kama kielelezo cha toba na wongofu
wa ndani. Watawa wanakumbushwa kumwilisha matendo ya huruma katika maisha na utume
wao, kama njia ya ushuhuda wa uwepo endelevu wa Mungu kati ya watu wake. Mama Kanisa,
anapenda kutoa shukrani na pongezi kwa watawa waliotawanyika sehemu mbali mbali za
dunia kutokana na majitoleo yao ya matendo ya huruma kwa maskini na wale wanaoishi
vijijini.
Inasikitisha kuona kwamba, idadi ya watawa inazidi kupungua mwaka
hadi mwaka, hasa katika nchi za Ulaya, hali ambayo inasababisha pia machungu katika
utoaji wa ushuhuda makini. Ufaransa ni kati ya nchi ambazo idadi ya miito na maisha
ya kitawa inazidi kupungua kwa kasi ya ajabu. Matatizo, changamoto na fursa zote hizi
zitumiwe kikamilifu na Mama Kanisa katika kuchunguza dhamiri ili kuona ni wapi ambapo
mambo hayakwenda vyema kadiri ya mpango wa Mungu, ili kujiwekea mikakati ya kuboresha
hali kama hii, kwa ajili ya mafao na ustawi wa Mama Kanisa kwa siku za usoni.
Ikumbukwe
kwamba, kila mwamini anawajibika kupandikiza mbegu ya miito mbali mbali ndani ya Kanisa
kwa njia ya ushuhuda wa maisha adili na matakatifu. Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi
na sita, kwa namna ya pekee, anawaalika watawa kutolea ushuhuda wa tunu msingi za
Kiinjili katika maisha na utume wao; maisha yao hayana budi kwenda sanjari na uhalisia
wa maisha wanayoyatangaza mbele ya watu.