Youcat: inavyochambua mafumbo ya imani ya Kanisa Katoliki kwa ajili ya vijana
Ninayo furaha kubwa kukukaribisha tena katika hema letu la vijana leo hii tunapoendelea
kuzipembua kurasa za ‘Youcat’, Katekesimu kwa Vijana ambayo Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita, kapenda kutuandalia. Wiki iliyopita tuliona ni kwa nini binadamu
anakuwa na uwezo wa kuamini. Leo hii tutaitazama
sehemu ya pili ya mada ya kwanza, ambapo Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita,
anatufundisha juu ya mafumbo makuu ya imani yetu. Ni mafumbo si kwa sababu ni mambo
ya maficho tusiyoweza kuyafahamu, bali ni mambo ambayo tunayafahamu ila kwa akili
ya kibanadamu hatuwezi kuyafahamu katika ukamilifu wake mpaka pale tutakapokutana
na Mungu mwenyewe uso kwa uso ndipo tutaweza kuyafahamu katika ukamilifu wake. Kanisa
limetupatia kanuni ya imani ambamo kuna mafumbo makuu ya imani yetu, baada ya kukili
imani tunaitikia AMINA, ishara ya kuyakubali kwa uhuru yale tuliyoyakili. Mafumbo
haya tunayokili si maneno au porojo tu za kijiweni, bali ni mambo halisi. Kanisa limeiweka
kanuni hii ya imani ili itusaidie kutafakari, kukiri, kujifunza, kurithisha kwa wengine,
kuadhimisha na kuyaishi mafumbo haya ya imani yetu. Kanuni ya imani inatusaidia
ili tusiamini wala kutangaza uzushi. Kwa hivi inatusaidia kukiri imani yetu kwa pamoja
kama asemavyo mt Ireneo wa Lyon ya kuwa kanisa linailinda imani kama vile linaishi
katika nyumba moja, na linaamini kama vile lina roho moja na moyo mmoja, nalo linaitangaza,
linaifundisha na kuirithisha kwa wengine kama vile lina kinywa kimoja. Tunasadiki
kwa Mungu mmoja, baba mwenyezi, muumba wa mbingu na nchi na vitu vyote vinavyoonekana
na visivyoonekana. Mungu ni mmoja katika nafsi tatu, yaani baba, mwana na roho mtakatifu.
Mungu si mpweke, bali anaishi kwenye umoja mkamilifu wa upendo katika utatu mtakatifu,
kwani Mungu ni Upendo (IYohane 4,8; 16). Mt. Augustino anatufundisha kuwa palipo na
upendo lazima pawe na utatu, yaani mwenye kupenda, mwenye kupendwa na chanzo chenyewe
cha upendo. Tunamwita Mungu baba mwenyezi sababu ndiye muumba wa vyote na anatujali
wote kwa upendo wa kibaba, hata Kristo mwenyewe katufundisha kumwita baba (Mathayo
6,9) na kama anavyotufundisha mtakatifu Paulo ya kuwa sisi tumeipokea roho ya kufanywa
wana, ambayo kwa hiyo twalia Aba, yaani baba (Warumi 8,15). Mungu ni muumba kwa sababu
vitu vyote vimetokana na utendaji wake. Kuhusu nadharia juu ya ubadilikaji au
ukuaji wa kimaumbile, kwa mtazamo wetu wa kikristo ni kwamba hata katika mabadiliko
hayo ni kazi ya Mungu mwenyewe ambayo inaendelea kupitia maumbile. Mungu kaumba vitu
tunavyoviona mfano mbingu, ardhi, maji n.k; na kaumba pia vitu tusivyoviona mfano
pumzi au roho. Tunaamini kwa Yesu Kristo, Mungu kweli na mtu kweli, mkombozi wa
ulimwengu. Aliyetungwa mimba kwa uwezo wa roho mtakatifu na akazaliwa na bikira Maria.
Na ili kutuokoa kutoka katika utumwa wa dhambi baada ya kuanguka kwa wazazi wetu wa
kwanza, ilimlazimu kusulubiwa msalabani. Siku ya tatu, Mungu akamfufua kutoka wafu
kama mzao wa kwanza wa waliolala mauti. Kristo katuonesha upendo mkuu na wa ajabu,
yaani nia ya Mungu kuishi na mwanadamu na utayari wake kusulubiwa na kukionja kifo
ili kutukomboa. Kristo katufundisha ni jinsi gani tunapaswa kuishi kama wanadamu ili
tuweze kuishiriki mbingu. Amepaa kwenda mbinguni na ameketi kuume kwa Baba naye
atarudi tena kwa hukumu ya mwisho. Mbingu si mahali bali ni hali ile ya kuwa katika
umoja na upendo na mwenyezi Mungu. Kila mmoja napofariki roho yake hupata hukumu binafsi,
na katika ile hukumu ya mwisho atakapokuja tena Kristo, kutakuwa na hukumu ya jumla
kwa ulimwengu mzima. Tunaamini kuwa Bikira Maria ni Mama wa Mungu, maana ni kwa uwezo
wa Roho Mtakatifu kampokea yesu katika tumbo lake la uzazi, Kristo aliye Mwana wa
Mungu. Yeye hakuwahi kumjua mwanaume. Sababu kwa pamoja na mchumba wake Yosefu,
Baba mlishi wa Yesu Kristo, walipenda kuishi hivyo maisha yao yote. Bikira Maria kwa
neema ya pekee na kwa mapenzi ya mwenyezi Mungu na kwa mastahili ya Kristo mwanae
mkombozi wa ulimwengu alikingiwa dhambi ya asili ili asiwe na doa la dhambi. Mpenzi
msikilizaji, ni kama vile unapofikia katika utamu wenyewe wa utafunaji mua, inakuwa
ngumu kuuachia. Ndivyo tulivyo kwa sasa tupo katika uhondo wenyewe wa kuyachambua
mafumbo ya imani yetu kama anavyotufundisha baba mtakatifu. Lakini kama unavyojua
mambo mazuri hayahitaji haraka, na ukitaka kujipa raha jitulize. Ni taaaaratibu
nikiondoka kwa mwendo wa kinyoga mpaka hapo wiki ijayo katika mida na nyakati kama
hizi, si mwingine bali mhudumu wa Altare ya Bwana Celestin Nyanda.