Kardinali Agustin Garcia-Gasco Vicente, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Valencia,
Hispania, afariki dunia
Mei Mosi, 2011, wakati Mama Kanisa anaimba utenzi wa shukrani kwa kutangazwa Mtumishi
wa Mungu Yohane Paulo wa pili kuwa Mwenyeheri, hapa mjini Vatican, furaha hii iligubikwa
na majonzi ya kifo cha Kardinali Agustin Garcia-Gasco Vicente, Askofu mkuu mstaafu
wa Jimbo kuu la Valencia, Hispania, aliyekuwa na umri wa miaka themanini. Alizaliwa
tarehe 12 Februari, 1931, Jimbo kuu la Toledo. Tarehe 26 Mei 1956 akapewa daraja
takatifu la Upadre.
Kunako tarehe 20 Marchi, 1985, Hayati Baba Mtakatifu Yohane
Paulo wa pili, akamteuwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Madrid. Tarehe 24 Julai,
1992 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Valencia. Katika maisha yake, aliwahi
kuwa mjumbe wa Tume ya Baraza la Kipapa la Familia; mjumbe wa Baraza la Kipapa la
Mafundisho Sadikifu na nidhamu ya Sakramenti za Kanisa.
Kunako Mwaka 2006,
Jimbo kuu la Valencia lilikuwa ni mwenyeji wa Mkutano wa Familia Kimataifa, uliohitimishwa
kwa uwepo wa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kuanzia tarehe 8 hadi 9 Julai,
2006. Akateliwa na Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kuwa Kardinali hapo tarehe
24 Novemba, 2007.