2011-04-22 07:57:08

Ijumaa Kuu: "Mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni"


Mama Kanisa siku ya Ijumaa kuu anatafakari kwa kina mateso ya Yesu Kristo Msalabani, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kutetea: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mheshimiwa Padre Alcuin Nyirenda anahitimisha tafakari ya kina katika Juma hili takatifu kwa kibwagizo kifuatacho "mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni". RealAudioMP3

Ndugu zangu, Siku kuu ya Pasaka ni kubwa sana, kudhihirisha uzito huo, tumepewa kipindi kizima cha siku arobaini, (kwaresima) kujiandaa ili tuweze kujipatanisha na Mungu. Katika kipindi hicho cha kwaresima tumevisikia vituko mbalimbali vilivyopelekesha Yesu kusakwa hadi kushikwa, halafu kumtesa, na kumhukumu, na kumnyonga msalabani hadi kufa.

Katika juma hili kuu, tumeona mambo mbalimbali yanayokera na kukirihisha sana moyo aliyotendewa Yesu na waumini wa dini wakiwa makuhani na wafuasi wake. Unaweza kubunia ni kosa gani la jinai alilolifanya Yesu hadi akastahili adhabu kifo? Alitenda kosa gani lililowakasirisha watu wengi hivi hata ikabidi kufanyike hata msako wa kumwua bila kuthamini uhai wake? Hivi Yesu alifanya tendo gani bovu hadi rafiki zake wakamsaliti?

Alifanya tendo gani la jinai hadi watu waliobobea kwa imani ya dini yao waweze kuvunja amri ya Mungu wao ya kutesa na kuua? Hakuna ambaye angeweza kufikiria kwamba maisha ya Yesu hapa duniani yangetamatika hivyo. Vitendo alivyotendewa Yesu na maneno ya karaha aliyonenewa Yesu ambayo yanakera katika Injili ya leo ni kwanza Yesu kuzabwa kofi, halafu na lugha aliyopewa na mtumishi wa kuhani. Ninashindwa kupata picha, namna gani binadamu anathubutu kumzaba kofi Mungu, mwumbaji wake, Bwana Yesu Kristu, aliyekuwa daima mwenye upendo na huruma kwa watu wote hapa duniani.

Hebu leo tulione suala hili la Yesu kupigwa kofi. mazingira yepi yaliyompelekesha Yesu hadi akazabwa kofi? Yesu baada ya kukamatwa alipelekwa moja kwa moja kwa kuhani Anasi ambaye Yohane anasema alikuwa ni mkwe wa kuhani mkuu Kayafa. Yaonekana makuhani hawa walikuwa pia na madaraka fulani ya kiserikali kadiri ya sheria ya warumi, ndiyo maana walipelekewa mhalifu kama Yesu ili wamhoji. Waliofaulu kuingia ndani alikokuwa kuhani ni Yohani kwa sababu alijulikana na kuhani (labda walikuwa ndugu), wengine kama Petro walibaki nje wanaota moto.

Kuhani alipomwuliza Yesu juu ya sera zake na juu ya wafuasi wake. Jibu la Yesu lilikuwa dhahiri kabisa kwamba yeye sera na mafundisho yake makuu ya ufunuo yalikuwa ya hadhara. Sera zake alikuwa anazimwaga pale anapoona imekusanyika lukuki ya watu, hivi hakuna mficho wala ubaguzi, ndivyo alivyoweza kupeleka ujumbe wake wa ukweli na haki kwa watu wote bila kuogopa dola wala dini ya mtu. “Mimi nimesema na ulimwengu waziwazi…wala sikusema neno lolote kwa siri. Ya nini kuniuliza mimi? Waulize wale waliosikia niliyowaambia; wao wanajua niliyoyanena.” (Yoh. 18:21).

Maneno haya ndiyo yaliyomchefua nyongo mtumishi mmoja ambaye kutokana na ushabiki na unafiki kwa Kuhani, akamzaba Yesu kofi, na kumwonya “Ndiyo majibu hayo kwa kuhani mkuu?” Hapa Yesu anashindwa kunyamaa kudhalilishwa na kunyongewa hivi haki yake ya kusema ukweli na haki anaona bora akanyweshe katumishi haka vidonge vyake. Jibu la Yesu la heshima ni fundisho kuu na laweza kuwa maelezo kwa msemo huu: “Mnyonge umnyongee lakini haki yake mpe. “Kama nimesema vibaya, ushuhudie ule ubaya; bali kama nimesema vema, wanipigia nini?” Hapa Yesu hakatai kupigwa kofi, maana alisema “mmoja akikupiga kofi la mkono wa kushoto mgeuzie na la kuume” (Mt. 5:39; Lk. 629).

Hapa lakini, Yesu anataka kuonyesha kwamba kipigo alichopata ni uhalifu, uhasama, uonezi, ametendewa jeuri kutokana na unyonge wa kutoweza kujitetea kwa vile amefungwa. Lakini ukweli hana kosa lolote. Hivi ndivyo wanavyotendewa wanyonge wasioweza kujitetea. Yesu anataka kuonyesha kwamba mnyonge yabidi atambuliwe daima na popote. Tendo lolote la ubabe dhidi ya mnyonge ni matumizi mabovu ya madaraka na mamlaka. Hivi anamwalika kijana kutumia akili yake na kutoa hoja kabla ya kuwaonea wanyonge: “Kama nimesema vibaya, ushuhudie ule ubaya”.
Tamko hili la Yesu kwa undani wake ni kama “kugeuza shavu la pili”, yaani, amesamehe lakini kusamehe huko hakufuti tendo aliloishatendewa. Halafu Yesu anaendelea kuuliza swali, “kama nimesema vema, wanipigia nini? Maneno haya yanawaendea wengi, yanamwendea Askari aliyemtenda vibaya, wale waliomhukumu kufa. Sanasana ni mwaliko kwenye tafakari juu ya kukoseana haki na juu ya udhulumu usioweza kuelezeka dhidi ya wanyonge.

Imepita tayari miaka elfu mbili na ushehe toka Yesu alipouliza swali hili: “Kwa nini wanipiga?” Swali hili linatoa nguvu kwa watu wote kutetea haki na ukweli vinapovunjwa, iwe katika familia katika serikali, katika dini, hasahasa dhidi ya wanyonge. Msimamo wa Yesu dhidi ya wanyonge na umuhimu wa kuizungumzia misingi ya haki za binadamu ndiyo jibu lililo kwenye roho ya ndani kabisa ya kusamehe ya upendo ambayo tunaikuta katika Injili ya leo.

Kwa vyovyote hata ukijua kusamehe na kupenda huko hakumaanishi kuukana uonevu na kukoseana haki ambako kunasababisha uovu. Msimamo huo wa Yesu una maana sana katika maisha yetu: yaani kuwatetea maskini, wadhaifu, wanyonge, wale wote wanaolowa damu kutokana na kudhulumiwa na viongozi na mataifa makubwa. Haitoshi tu kuwatetea wanyonge, bali yabidi pia kutetea haki, yaani haki ya kila mmoja na siyo kusubiri hadi yatokee madhulumu na uonezi wa hao wakuu ufanyike ndipo tuanze kutangaza uhuru na kuheshimiana na kujaliana.

Mateso ya Yesu ni hasa kule kugandamizwa na maamuzi ya kikandamizaji yasiyojali utu wa mtu, hata kama mtu huyo ni mnyonge na asiye na hatia yoyote kabisa, lakini ananyongewa na kuuawa. Swali la Yesu linagusa moja kwa moja dhamira ya kila mtu mwenye mapenzi mema (wa kila dini ya kweli), la kutetea heshima na haki ya wanyonge.

Leo Yesu anatuuliza sisi swali hilo. “Kwa nini wanipiga?” Endapo hatumpigi mwilini, je tunajeruhi Moyo wake Mtakatifu kutokana na kushindwa kukabiliana na uovu wa ulimwengu? Je, hatumpigi Yesu usoni pale tunaposhindwa kuwaonyesha upendo wengine? Je, hatumnyimi chakula Yesu pale tunaposhindwa kuwapa chakula wenye njaa. Je, hatumfukuzi Yesu, pale tunaposhindwa kuwakaribisha wageni? Tunaposhindwa kuwahudumia wagonjwa na kwenda kuwaona wafungwa?

Ndugu zangu, Yesu alisema: “Kweli nawaambieni, yeyote mliyomtendea mmoja wa ndugu zangu, mmenitendea mimi.”[Mt. 25:40] Je, wiki iliyopita, au mwezi na mwaka uliopita ulimpiga Yesu? Tusiwaonee wanyongee kwani tunajitia wenyewe upumbavu na kushindwa kujibu swali la Yesu “wanipigia nini?”. ndivyo, basi tujionee huruma wenyewe! Yesu ni mwenye huruma daima, tumebahatika naye kupewa Sakramenti ya Kitubio tunamoweza kwenda kusafisha mioyo yetu iliyochafuka kutokana na uovu tulioutenda dhidi yake.

Leo na kesho, Kanisa linatupendekezea kufunga kwa ajili ya kushiriki mateso na kifo cha Bwana Yesu, ili kujiandaa wenyewe vizuri kushiriki kikamilifu na kwa dhati furaha na utukufu wa Ufufuko.








All the contents on this site are copyrighted ©.