2011-03-29 08:57:33

Jubilee ya miaka 80 ya Radio Vatican na changamoto zake!


Radio Vatican inaendelea kuadhimisha Jubilee ya miaka themanini tangu ilipoanzishwa kunako mwaka 1931 hadi leo hii mwaka 2011. Hayati baba Mtakatifu Pio wa kumi na moja, ndiye aliyekuwa Khalifa wa kwanza wa Mtakatifu Petro kuzungumza moja kwa moja kupitia Radio Vatican baada ya kuanzishwa kwake na Bwana Guglielmo Marconi, huo ukawa ni mwanzo wa Radio Vatican, iliyoanza kurusha matangazo yake kwa lugha nane zinazotumika hususan Barani Ulaya. Wakati wa vita kuu ya pili ya dunia, Radio Vatican ilikuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba inatoa habari kwa wakimbizi na wafungwa wa kisiasa wakati huo. RealAudioMP3

Kunako mwaka 1957 Radio Vatican ikaanza kutoa taarifa ya habari sanjari na maendeleo ya sayansi ya teknolojia yaliyoiwezesha Radio Vatican kurusha matangazo yake Barani Afrika, Asia na Amerika kwa kutumia Masafa Mafupi. Mnara wa matangazo haya ulizinduliwa kunako mwaka 1957 na Baba Mtakatifu Pio wa kumi na mbili.

Wakati wa Mtaguso mkuu wa pili wa Vatican, Mababa wa Mtaguso walikuwa bega kwa bega na Radio Vatican kuhakikisha kwamba, ujumbe wa Mtaguso mkuu wa pili wa Vatican unawafikia walengwa kwa wakati muafaka. Radio Vatican iliweza kutangaza kwa lugha thelathini kwa mkupuo. Kunako mwaka 1970, Makao Makuu Mapya ya Radio Vatican yalifunguliwa ili kuwezesha idara mbali mbali kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa zaidi. Tangu wakati huo, Radio Vatican ikaanza kurusha matangazo yake kwa lugha thelathini na mbili.

Mwaka 1993 Radio Vatican ilianza kurusha matangazo yake kwa njia ya Satelite. Maendeleo haya ya Sayansi na Teknolojia ya Habari yaliiwezesha Radio Vatican kunako mwaka 1998 kuanza kurusha matangazo yake kwa mtindo mpya wa digital. Maadhimisho ya Jubilee kuu ya miaka elfu mbili ya Ukristo, lilikuwa ni tukio ambalo liliiwezesha Radio Vatican kuwafikia watu mbali mbali, si tu kwa njia ya sauti, bali watumiaji wa mtandao waliweza pia kupata maandishi na kufanya rejea ya kile kinachotangazwa.

Kunako mwaka 2005, kifo cha Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili na kuchaguliwa kwa Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, kuliongoza Kanisa Katoliki, kulileta mabadiliko makubwa katika matangazo ya Radio Vatican, kwani tangu wakati huo, Radio Vatican ilifungua mtandao wake unaobeba lugha thelathini, ili kuwafikia walengwa millioni moja na nusu. Hadi sasa Radio Vatican inashirikiana kwa karibu zaidi na Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV, ili kuhakikisha kwamba, watu wanaweza kusikiliza, kuona na kusoma kile kinachozungumzwa, kinachorushwa na kuandikwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Hadi sasa kuna jumla ya lugha thelathini na nane zilizoko kwenye Ukurasa wa Mtandao wa Radio Vatican, bila kusahau lugha ya Kiswahili inayoendelea kuboresha mtandao wake, ili kuwanufaisha wasikilizaji na wasomaji wake. Radio Vatican ina jumla ya wafanyakazi mia tatu na hamsini na tano, kati yao wanaume ni mia mbili na arobaini, wakati ambapo wanawake ni mia moja na kumi na tano. Wafanyakazi hawa wanatoka katika mataifa hamsini na tisa; wote huu ni utajiri unaofumbatwa ndani ya Radio Vatican.

Gharama za kuendesha Radio Vatican kwa mwaka zinafikia kiasi cha takribani Euro millioni ishirini na tano. Kwa miaka zaidi ya sabini na tisa, Radio Vatican iliendeshwa kwa gharama za Vatican, lakini sasa, imeanza kuruhusu matangazo ya biashara, ili kujenga hatua kwwa hatua uwezo wa kuchangia gharama za uendeshaji wa shughuli zake.

Ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari, Radio Vatican inaendelea kuboresha pia huduma zake kwa kuhakikisha kwamba, inakuwa na rasilimali watu wa kutosha kukabiliana na changamoto hizi.

Hivi karibuni, Idhaa ya Kiingereza na Kiswahili ya Radio Vatican imepata mdau mpya atakashikilia Jahazi katika kipindi hiki cha mageuzi makubwa naye ni Padre Moses Hamungole kutoka Jimbo kuu la Lusaka, Zambia, aliyepadrishwa kunako mwaka 1994.

Ni mtu mwenye uzoefu mkubwa katika masuala ya maendeleo ya teknolojia ya habari, kwani tangu mwanzo wa utume wake, amefanya kazi katika Idara ya Habari Baraza la Maaskofu katoliki Zambia, baadaye akahamishiwa Nairobi, kwenye Makao Makuu ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA. Amewahi kuwa ni Rais wa Signis, Afrika na Mjumbe wa Bodi ya Signis kwa kipindi cha miaka minne.

Akizungumza katika hafla ya utambulisho wa Padre Moses Hamungole, Padre Andrea Koprowski, Mkurugenzi wa Vipindi, Radio Vatican alimshukuru kwa namna ya pekee, Beth Hay ambaye ameongoza Idhaa ya Kiingereza na Kiswahili kwa takribani miaka ishirini, hadi kufikia mafanikio yaliopo kwa sasa. Lakini Radio Vatican inaendelea kukabiliana na changamoto mbali mbali na mang’amuzi yake kama chombo cha mawasiliano cha Kanisa Katoliki duniani.

Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika ilileta changamoto ya pekee katika mbinu mkakati wa Radio Vatican, kiasi cha kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Kanisa Barani Afrika; kwa ajili ya mafao ya Kanisa na maendeleo endelevu ya watu wa Afrika. Radio Vatican katika mtandao wake, ikaanzisha ukurasa wa pekee ambao umekusanya hati mbali mbali zilizotolewa wakati wa maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika, hati ambazo hadi leo hii mtu anaweza kufanya rejea kwani zinapatikana katika mtandao. Radio pia imeanzisha Ramani ya Afrika inayokusanya na kutunza habari mbali mbali zinazopatikana kutoka Afrika.

Padre Moses Hamungole anakuja katika kipindi hiki cha mabadiliko makubwa ndani ya Radio Vatican. Yeye atakuwa ni kati ya wale wanaounda Kikosi kazi kinachopania kuboresha kurasa za mtandao wa Radio Vatican Barani Afrika, Asia na Ulaya. Dhamira ya Radio Vatican ni kuendelea kuwa ni daraja la habari kati ya Vatican na Kanisa Barani Afrika, kwa kuwa na uhakika na usahihi wa habari kutoka Afrika.

Padre Hamungole ana haya ya kusema wakati huu: “Ninapenda kumshukuru Mungu kwa kunijalia nafasi hii ya kuweza kushirikisha kile kidogo ninachokifahamu kwa ajili ya mafao na maendeleo ya Kanisa Barani Afrika katika ulimwengu wa habari. Kwa namna ya pekee, ninaushukuru uongozi wa Radio Vatican, kwa kuniona na kunialika ili kuwa ni sehemu ya wadau wa habari kwa ajili ya Kanisa la kiulimwengu, lakini kwa namna ya pekee, Kanisa Barani Afrika. Ninamshukuru kwa namna ya pekee Beth Hay kwa ukarimu na ushirikiano alionionesha tangu nilipowasili hapa Radio Vatican. Nina uzoefu wa maisha na utume wa kipadre kwa takribani miaka kumi na saba."

Ni matumaini yangu kwamba, uzoefu na mang’amuzi haya yatanisaidia kujenga kikosi kazi kwa ajili ya kuboresha matangazo ya Radio Vatican kwa Bara la Afrika. Lengo la kufanya kazi kwa ushirikiano na mshikamano wa dhati ni kujenga udugu, amani, upendo na matumaini kati ya watu, ili kwa pamoja, tuweze kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika ulimwengu wa maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari duniani. Hili ni jukumu linalohitaji sadaka na majitoleo ya mtu binafasi na kama kikosi kazi, ili kuleta mvuto katika utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu kwa sehemu mbali mbali za Afrika.

Ni changamoto ya kila mtu kutumia kikamilifu vipaji vyake kwa sifa na utukufu wa Mungu, mintarafu vipaumbele vya Radio Vatican. Ninapoanza utume wangu hapa Radio Vatican, ninahitaji ushirikiano na mshikamano wa dhati na kila mfanyakazi. Nitaendelea kujifunza kadiri ya wakati, ili kutekeleza vyema wajibu wangu.”








All the contents on this site are copyrighted ©.