Nabii ni rafiki wa watu, msimamizi wa ukweli, mtu wa huzuni na mateso!
Jandokasisi Celestini Nyanda toka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, kilicho mjini
Roma, anaendelea kupembua dhamana ya Kanisa Barani Afrika katika mchakato wa kudumisha:
haki, amani na upatanisho, mintarafu nafasi ya Nabii katika jamii.
Itakumbukwa
kwamba, amekwisha zungumzia kuhusu: Nabii kama mjumbe wa Neno la Mungu, Mtumishi wa
Bwana, Mtu wa Mungu na Mlinzi katika jamii. Katika makala haya anaendelea kumwangalia
Nabii kama rafiki wa watu, msimamizi wa tunu ya ukweli, mtu wa huzuni na mateso.
Rafiki wa
Watu:
Nabii anakuwa ni rafiki wa watu kwani mahusiano ya nabii na Mwenyezi
Mungu hayamtengi na jamii anamoishi bali yanamsogeza karibu zaidi nao, ili aweze kuyatambua
vema maisha yao na kuwasaidia. Waamini wanapaswa kujenga mahusiano ya urafiki wa
kweli katika jamii. Kwa namna hii wanaweza kuyatambua vema maisha ya wanajumuiya kwa
ujumla, na hivi kuyagundua maovu yaliyofichika ndani humo na kuyatafutia tiba thabiti
kutoka kwa Kristo aliye tabibu wa kweli wa kila baya. Mahusiano ya mkristo na Wana
wote wa Mungu yanamjengea pia hali ya upendo na ya kujali.
Hii haimaanishi
kuwapenda watu na jamii yake na kuyafunika maovu yao, kwani huu hauwezi kuwa upendo
wa kweli. Na pia kwa sababu nabii siku zote anasimamia neno la Mungu, vinginevyo atakuwa
nabii wa uongo. Ndivyo anavyokuwa mpatanishi kati ya watu na Mwenyezi Mungu kama alivyofanya
Kristo mwenyewe. Kristo kautwaa mwili wa mwanadamu, na akaisha kati yetu ili kuzifahamu
taabu na raha zetu, akatufanya marafiki wake na akatupatanisha na Mungu Baba. Na sasa
anaendelea kutuombea akiwa ameketi kuumeni mwa kiti cha Enzi cha Baba.
Ni
wajibu wetu wabatizwa barani Afrika kuwa waombezi wa jumuiya tunamoishi kwa mfano
wa nabii Musa jinsi alivyokuwa mwombezi na mpatanishi wa wana wa Israeli na Mungu
Baba. Sala ya mtu mwema ina nguvu ya kutenda makuu. Kwa hivi muumini mwadilifu na
mwenye haki anapotolea maombi ya kweli, sala yake inasikilizwa na Mwenyezi Mungu,
naye hutenda kwa wakati wake.
Haki, amani na upatanisho Barani Afrika vitapatikana
iwapo: waamini watakuwa mawakili wa kweli wa Kristo katika kutafuta maelewano kwa
njia za halali na kukesha katika sala ili kuliombea Bara letu ambalo kwa muda mrefu
linasongwa na mawimbi makali ya unyanyasaji na umwagaji damu na migogoro mikubwa.
Bwana Yesu mwenyewe anatufundisha ya kuwa, aina nyingine za magumu na mabaya hazitafutiwi
ufumbuzi kwa urahisi bila kusindikizwa kwa sala na kufunga.
Katika kuyafunua
maovu na kuionya jamii, yampasa nabii mwenyewe kuachana na uovu huo. Kwa sababu hiyo
waamini wakristo barani Afrika wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kutenda haki,
kutafuta amani na kukuza mapatano ya kweli “heri wenye njaa na kiu ya haki, maana
hao watashibishwa” (Mathayo 5,6).
Msimamizi wa Ukweli:
Katika jamii
anamoishi na anayoihudumia na kuitolea ushuhuda, nabii ni mtu wa ukweli. Yeye anaishi
katika kweli, na anaitangaza kweli ya Mungu. Sababu hiyo anapoyaona maovu, hatari
au mwelekeo wowote mbaya katika jamii, anauweka wazi ukweli na hali halisi ya jamii.
Nabii anapingana na manabii wa uongo: wenye kudanganya watu kuwa kila kitu kiko sawa;
kuwapa ahadi za uongo au baraka zisizo na misingi ya imani ya kweli; wenye kuwaahidia
watu miujiza na maisha rahisirahisi yasiyo na kweli yoyote ndani yake.
Katika
hali hii, nabii anasimama kidete kuutetea ukweli bila kuficha kama anavyofanya nabii
Yeremia akiwafikishia ujumbe wana wa Mungu na kuwaonya kwa maneno ya Bwana mwenyewe
anayesema “wameliponya jeraha la watu wangu kwa juu juu tu, wakisema Amani Amani na
wakati hapana Amani” (Yeremia 6,14). Ndivyo wanavyoalikwa waamini wa Kristo Barani
Afrika, kuusimamia ukweli katika kila hali, kutodanganyika na ahadi za uongo na hivi
kuyaweka mambo wazi ili kuyatafutia ufumbuzi.
Mtu wa Huzuni na Mateso:
Katika
utendaji na katika ushuhuda wake nabii anakumbana pia na magumu mbalimbali. Anakumbana
na magumu sababu baadhi ya watu hawauamini na kuupokea ukweli kwa urahisi, sababu
baadhi yao wanawachukulia manabii kama chanzo cha kuwavurugia maisha ya starehe, au
hata kuwadhani kuwa ndio chanzo cha mvurugano na taabu katika jamii. Wakati mwingine
hata kuwatesa manabii wa Mungu ili waache kuuhubiri ujumbe wa Mungu. Hali hii hupelekea
mara nyingi kumfanya nabii kuwa mtu wa mateso na huzuni nyingi.
Waamini Barani
Afrika wamekutana na hali kama hizo na bado wanaendelea kukutana nazo. Manabii hawa
barani Afrika hawawezi kutishwa wala kuzuiwa kwa mateso hata kifo. Kwa kuwa wamekuwa
tayari tangu awali kuisimamia kweli na imani yao hata mwisho, hata ikiwalazimu kumwaga
damu yao kwa kumshuhudia Kristo na kuisimamia kweli kama walivyofanya watakatifu Karoli
Lwanga na wenzake, mtakatifu Bakhita, mwenye heri Bakanja na wengine wengi barani
Afrika.
Hitimisho, Wokovu wa bara la Afrika unategemea sana uinjilishaji
wa kina. Ujumbe unaoenezwa kwa utume wa kinabii, wanaoubeba waamini wote waliobatizwa
katika Kristo Yesu, Mfalme wa Haki na Amani.