Askofu Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar asema: utamadunisho ni changamoto inayolikabilia
Kanisa Barani Afrika
Mababa wa Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu, katika mapendekezo yao kwa Baba Mtakatifu
Benedikto wa kumi na sita anayoendelea kuyafanyia kazi, ili hapo mwakani, Mwezi Novemba,
aweze kutangaza matunda ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu wa Afrika, walilaani
na kukemea vikali mila na desturi mbaya Barani Afrika ambazo zimepelekea kuvunjika
kwa misingi bora ya utu na maadili mema. Wanaendelea kukazia majadiliano ya kidini
na kiekumene kama njia ya kujenga haki, amani, upendo na mshikamano wa dhati ndani
ya jamii. Wanalaani na kukemea misimamo mikali ya kiimani, ambayo imepelekea mara
nyingi kuvunjika kwa amani na upendo kati ya watu.
Mababa wa Sinodi wanaendelea
kuhimiza umuhimu wa Uinjilishaji kwa njia ya ushuhuda wa maisha na tunu msingi za
kikristo kwa kukazia: uwazi, ukweli na kuheshimiana pamoja, sanjari na mchakato wa
majadiliano ya dhati yanayozingatia kweli za Kiinjili. Kanisa Barani Afrika linajitambua
kuwa ni Familia ya Mungu inayowajibika, changamoto kubwa ni kuhakikisha kwamba, linaendelea
kuwa ni kielelezo amini cha upatanisho, haki na amani; kuwa kweli ni chumvi ya dunia
na mwanga wa mataifa.
Askofu Augustine Ndeliakyama Shao wa Jimbo Katoliki Zanzibar
katika mahojiano na Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican anasema utamadunisho ndani
ya Kanisa Barani Afrika ni dhana au mchakato unaoweza kuwasaidia waamini kuweka misimamo
ya maisha ya kidini na kiimani katika uhalisia wake; kwa kuchukua tunu njema, mila,
desturi na tamaduni nzuri toka katika maisha ya kiafrika na kuzimwilisha kadiri ya
kweli za Kiinjili.
Anasema, mila, desturi na mapokeo potofu yaliyopitwa na
wakati, zinapaswa kuachwa, ili kukumbatia mwelekeo mpya wa Kiinjili, ili kuondokana
na dhana ya uwili katika maisha ya kikristo; ili hatimaye, kuwawezesha wakristo kutolea
ushuhuda imani yao katika medani mbali mbali za maisha.
Ili kufanikisha azma
hii, kuna haja ya kujenga misingi ya majadiliano ya kweli katika: dini kwa kujifunza
undani wa dini asilia kwani hii ni sehemu ya maisha ya watu wenyewe, bila kusahau
kuangalia mila na desturi za watu na maisha yao kwa ujumla. Lengo ni kukoleza dhana
ya utamadunisho ndani ya Kanisa. Ninakualika sasa kwa heshima na taadhima kubwa, ukae
kitako ili uweze kumsikiliza kwa makini Askofu Augustino Ndeliakyama Shao wa Jimbo
Katoliki Zanzibar katika akifafanua zaidi.