Mheshimiwa Sana Padre Sosthene Ayikuli Udjuwa ateuliwa kuwa Askofu wa Mahagi-Nioka,
DRC
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, amemteua Mheshimiwa Sana Padre Sosthene
Ayikuli Udjuwa, msimamizi wa kitume Jimbo Katoliki la Mahagi- Nioka kuwa Askofu mpya
wa Jimbo la Mahagi-Nioka, Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Congo.
Askofu
mteule Ayikuli Udjuwa, alizaliwa tarehe 7 Julai, 1963 huko Faradje. Baada ya masomo
yake ya shule za Sekondari, kati ya mwaka 1985 hadi 1988, aliendelea na majiundo ya
falsafa huko Kisangani na masomo ya kitaalimungu, aliyapatia huko Bunia, kati ya Mwaka
1988 hadi 1993. Tarehe 15 Julai, 1993 akapewa daraja takatifu ya Upadre.
Tangu
wakati huo, alibahatika kufanya kazi mbali mbali ikiwa ni pamoja na kufundisha Seminari
Ndogo ya Yohane wa Ishirini na tatu huko Mahagi-Nioka. Baadaye alijiendeleza kwa masomo
ya juu katika Sheria za Kanisa, Kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki, Kinshasa. Akawa
ni jaalimu wa Taalimungu kwenye Taasisi ya Mtakatifu Cyprian huko Bunia.
Baada
ya masomo yake ya uzamivu wa sheria za Kanisa, toka Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterani,
kilichopo mjini Roma, kunako mwaka 2009 alirudi nyumbani na kuteuliwa kuwa ni Msimamizi
wa Jimbo Katoliki la Mahagi-Nioka, DRC.