Watakatifu wapya wanalipamba Kanisa kwa mifano ya maisha yao na udumifu katika sala
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, Jumapili tarehe 17 Oktoba, 2010, kwenye
Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, uliofurika kwa waamini na mahujaji
kutoka pande mbali mbali za dunia, aliwatangaza wenyeheri sita kuwa watakatifu. Watakatifu
wapya wanaolipamba Kanisa kwa mifano ya maisha na udumifu wao katika sala ni: Stanislaw
Soltys Kazimierczyk, Andrè Bessette, Candida Maria De Jesùs Cipitria y Barriola, Mary
MacKillop, Julia Salzano na Battista Varano.
Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu
amekazia umuhimu wa kusali na kudumu katika sala, kama sehemu ya mafundisho msingi
ya Jumapili ya ishirini na tisa ya kipindi cha Mwaka wa Kanisa, kwa kutambua na kuendelea
kuthamini umuhimu wa sala katika maisha na utume wa Kanisa.
Baba Mtakatifu
anasema, kwa bahati mbaya watu wanadhani kwamba, kwa nguvu zao za kibinadamu bila
msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu wanaweza kufanikisha malengo yao. Ni changamoto kwa
waamini pia kuhakikisha kwamba wanakuwa ni watu wa haki kwa kutenda haki, hasa kwa
wanyonge na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha.
Baba Mtakatifu anawakumbhusha waamini kuwa: Mwenyezi Mungu ni kielelezo cha
ukarimu na huruma na daima yuko tayari kusikiliza kwa makini kilio cha waja wake katika
sala, changamoto kwa waamini kutokata tamaa katika sala, bali kujenga utamaduni wa
kudumu katika kusali, kama Kristo mwenyewe anavyohimiza. Sala katika undani wake ni
kielelezo cha imani katika wema wa Mungu anayemlipa kila mmoja kadiri anavyopenda.
Huu ni msingi wa maisha ya sala, kama inavyojionesha katika maisha ya watakatifu waliotangazwa
siku ya Jumapili kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican.
Mtakatifu
Stansilaus, mtawa aliyeishi kunako karne ya kumi na tani ni mfano wa mtu aliyeyamimina
maisha yake katika Ibada kwa Ekaristi Takatifu. Ni mtu aliyejifunza kutoka kwa wazazi
imani na maisha ya ibada; akawa mtawa; akatekeleza wajibu wake kama Padre na mwalimu,
akiwa makini zaidi kwa mahitaji ya watu maskini zaidi. Alionesha upendo wa pekee kwa
Kristo wa Ekaristi Takatifu, akamwona Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka, anayeendelea
kujitoa katika Sadaka ya Misa Takatifu, kama kielelezo na msukumo wa pekee kwa upendo
wa Mungu na jirani, chemchemi ya umoja.
Bruda Andrè Bessette alizaliwa nchini
Canada, mtawa wa Shirika la Msalaba Mtakatifu, ni mtu aliyeonja makali ya umaskini
katika utoto wake, akajifunza kumgeukia Mungu kwa maisha ya ndani zaidi, akawaonjesha
saburi wote waliotumaini maombezi yake. Kwa uelewa wake, alijitahidi kuyafahamu yale
yaliyokuwa msingi kwa ajili ya imani yake, akajifunza kujiachilia kutimiza mapenzi
ya Mungu katika maisha yake. Alijitahidi kumwilisha heri za Kiinjili katika maisha
yake kwa njia ya unyenyekevu kwa Mungu.
Ni mtu aliyefanikisha ujenzi wa Madhabau
ya Mtakatifu Yosefu, akawa mlinzi wake hadi mauti ilipomfika kunako mwaka 1937. Mahali
hapa akawa ni shahidi wa nguvu ya uponyaji na wongofu wa ndani, daima aliwahimiza
wakristo kuwa na subira katika majaribu ya maisha yao na kamwe wasiombe kuondolewa
bali waombe neema na baraka ya kuweza kuyabeba kwa imani na matumaini makubwa. Ni
mkristo aliyejitahidi kumfatuta Mungu katika unyenyekevu wa maisha yake ya kila siku,
changamoto kwa waamini kutoka Canada.
Mtakatifu Candida Maria, alikirimiwa
kuwa na fadhila ya unyenyekevu tangu mwanzo wa maisha yake, akabahatika kuwapata mapadre
waongozi wa kiroho kutoka Shirika la Wayesuiti, kiasi cha kumfanya kutoa kipaumbele
kwa Mwenyezi Mungu, akaendelea kuwa mwaminifu kwa Mungu hata alipoitupa mkono dunia.
Aliyatoa maisha yake kwa Mungu na akawaonjesha upendo wake wa dhati maskini na wote
waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii wakati huo. Akajitoa bila ya kujibakiza
kwa ajili ya majiundo ya wasichana na wanawake wa nyakati zake, kiasi cha kuwa ni
mwanzilishi wa Shirika lake, changamoto ya maisha kwa waamini wengine ndani ya Kanisa.
Mtakatifu
Maria MacKillop, enzi ya uhai wake, aliwahimiza waamini kuwatambua na kuwathamini
waalimu wao wa imani, waliowashirikisha hekima inayowakirimia wokovu na maisha ya
uzima wa milele. Baba Mtakatifu anasema, vijana wengi nchini Australia wamebahatika
kufundishwa na walimu wanaojitahidi kuiga mfano na ujasiri wa Mtakatifu huyu, kwani
hao ndio watawa waliojiunga naye katika harakati za kutoa elimu kwa watu maskini nchini
Australia.
Ni mwanamke aliyejitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya vijana waliokuwa
wamedhaminishwa kwake, bila kujali matabaka au utajiri wao, wote wakabahatika kupata
majiundo ya kiroho na kiakili.
Licha ya changamoto mbali mbali alizokumbana
nazo katika maisha yake, lakini, daima kwa njia sala alikimbilia maombezi ya Mtakatifu
Yosefu na akajifunza kujificha kwenye Ibada ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kiasi cha kuliweka
Shirika lake, chini ya ulinzi na usimamizi wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, akabahatika
kubaki mwaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, changamoto kwa waamini kujitoa bila ya
kujibakiza kwa ajili ya hudjma kwa Mungu na Kanisa kwa njia ya imani na unyenyekevu.
Julia
Salzano ni mwalimu wa shule ya msingi, aliyeishi kunako karne ya kumi na tisa, huko
Kusini mwa Italia, aliyeitwa kwa neema za Mungu kuwa ni mtume hodari wa Kanisa katika
sekta ya elimu, akabahatika pia kuwa ni mwanzilishi wa Shirika la Watawa Makatekista
wa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Ni mtu aliyetambua na kuthamini katekesi katika maisha
na utume wa Kanisa, akajitahidi kuunganisha mbinu za kufundishia, jambo lililomwezesha
kuwa na ari katika utume wake, akajitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya majiundo ya
watu wa kila umri na tabaka.
Ni mtawa aliyetamani kufundisha katekesi hadi
dakika yake ya mwisho ya maisha yake hapa duniani, kwa kutambua kwamba, Mungu alimuumba
mwanadamu ili amtambua, ampende na kumhudumia katika maisha yake, kama mambo yanayopaswa
kupewa kipaumbele katika maisha ya mwamini. Baba Mtakatifu anasema, mfano wa Mtakatifu
Julia Salzano ni changamoto kwa Mama Kanisa kuendelea kumtangaza Kristo sanjari na
kuunda dhamiri nyofu za waamini.
Mtakatifu Battista Camila Varano, ni mtawa
wa Shirika la Waklara aliyeishi kunako karne ya kumi na tano, kielelezo makini cha
ushuhuda wa maana ya maisha ya Kiinjili na udumifu katika sala. Akiwa na umri wa miaka
ishirini na tatu, akawa ni kati ya wakereketwa wa maisha na karama ya Mtakatifu Clara
wa Assis, akawa ni muasisi wa nyumba nyingine za kitawa na mkuu wa nyumba kwa nyakati
mbali mbali. Akajitoa biula ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, watawa na jirani zake
katika fadhila ya upendo, akijichotea baraka na nguvu katoka katika Moyo Mtakatifu
wa Yesu. Ni mtawa aliyeyachimbia maisha yake katika toba na sala, akijitahidi daima
kuleta mabadiliko ndani ya Kanisa.
Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita,
alihitimisha mahubiri yake, kwa kuwaalika waamini kumtolea Mwenyezi Mungu utenzi wa
shukrani kwa utakatifu wa maisha, unaoendelea kung'aa ndani ya Kanisa kwa njia ya
ushuhuda wa watakatifu wapaya waliotangazwa na Mama Kanisa siku ya jumapili. Ni changamoto
kwa waamini kuendelea kuongozwa na mfano wa maisha yao ili maisha ya kila mwamini
uwe ni utenzi wa sifa kwa Mwenyezi Mungu.