Utangazaji wa Neno la Mungu, Tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo na maisha ya Kijumuiya
changamoto kuu kwa viongozi wapya!
Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Vikarieti ya Tanzania, katika mkutano
wa uchaguzi mkuu, wamewachagua viongozi watakaoliongoza Shirika katika awamu ya nne,
kipindi cha mpito kuelekea ukomavu kamili, utakaoliwezesha Shirika kujitegemea katika
maisha na mikakati yake ya kichungaji.
Mheshimiwa Padre Felix Mushobozi, C.PP.S,
Katibu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Takatifu ya Yesu, kwa niaba ya Makao Makuu
ya Shirika, anawapongeza viongozi waliohitimisha muda wao wa kuliongoza Shirika na
kuwakaribisha viongozi wapya, akiwataka zaidi kujikita katika nguzo kuu tatu: Utangazaji
wa Neno la Mungu; tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo, itakayowawezesha wanashirika kusikiliza
na kujibu "Kilio cha damu" katika ulimwengu wa leo na kwamba, nguvu za kuweza kusonga
mbele katika maisha na utekelezaji wa mikakati yao ya kichungaji zinafumbatwa katika
maisha ya Kijumuiya katika msingi wa mshikamano wa upendo.
Mheshimiwa Padre
Felix Mushobozi anaendelea.
Mnamo tarehe
17 mwezi huu wa Juni, Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu walipokutana katika mkutano
mkuu wa Uchaguzi walimchagua Pd. Reginald Mroso kuwa Mkuu mpya wa shirika Tanzania.
Katika mkutano huo walichaguliwa washauri wake: Pd. Gregory Mkhotya kuwa naibu wake,
Pd. Eugene Nchimbi kuwa Katibu, Pd. Thomas Wambura katika nafasi ya uhasibu na Pd.
Egidius Seneda kama mshauri.
Kwa niaba ya Halmashauri ya Shirika Ulimwenguni
yenye makao makuu hapa mjini Roma, napenda kutoa salamu zangu za pongezi kwa kuteuliwa
kwao kulitumikia shirika katika sehemu hii ya Afrika. Ni takriban miaka kumi na miwili
toka sehemu hii ya shirika iwe Vikariati (yaani hatua moja kabla ya kuwa Province).
Nachukua nafasi hii kuwashukuru viongozi ambao walikuwa madarakani kwa jitihada
zao za kuhamasisha Wanashirika katika maisha ya jumuiya, katika kuendeleza tasaufi
ya Damu Azizi ya Yes una kuratibu mipango mabalimbali ya utume na uchungaji. Tunapoongea
sasa hivi Wamisionari wa Vikariati ya Tanzania wanafanya kazi katika nci mbali mbali
ulimwenguni: Italia, Amerika ya kaskazini (USA), Chile, Colombia na Guinea Bissau.
Kama kwa mamna moja shirika limepiga hatua katika kukomaa katika utambuzi
wa yale yanayotufanya kuwa Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, kv. Maisha ya jumuiya,
tasaufu ya Damu Azizi ya Bwana wetu Yesu Kristo na Umisionari; changamoto katika kuelekea
ukomavu endelevu bado ni nyingi.
Matamanio ya halmashauri ya shirika hapa makao
makuu ni kuona shirika katika Tanzania na mahali pengine tunapofanyakazi, linaendeleza
Karama tulizorithishwa na Mwasisi wetu Mt. Gaspari, yaani kuhubiri neno la Mungu,
hasa kuwasogeza watu wa Mungu karibu na Mto wa Rehema yaani Damu iliyomwagika Msalabani
wakaoshe mavazi yao yawe meupe tayari kumlaki Mwanakondoo atakapokuja siku ya Mwisho.
Uongozi ulio bora ni ule unaotafuta kutimiza lengo hili kwa ufanisi kwa kupanga
kimahiri na pamoja malengo na kuyatimiza kwa mshikamano mkuu. Kwa bahati njema, kadiri
ya katiba na kanuni zetu mamlaka katika shirika hayamo mikononi mwa viongozi bali
katika wanashirika wanapokaa na kupanga na kuamua maisha ya shirika kwa pamoja. Bila
shaka viongozi hawa waliochaguliwa wanatambua hili na ndio maana wamechaguliwa.
Kazi
yao itakuwa rahisi kama wataweza kutimiza vyema kazi ya kuwa viungo vya maisha ya
jumuiya, wakijitahidi kuwa “facilitators’ wa yale yaliyoamuliwa na wanashirika wakijitahidi
kuwa macho ya kuona mbele na kuwaongoza wanashirika wapange na kutimiza wajibu na
utume wao kwa uaminifu na ufanisi.
Kinyume cha hapo uongozi utakuwa mgumu
kama wakijaribu kufanya yote peke yao au kuweka pembeni yaliyoamuliwa na jumuiya na
kuamrisha yatimizwe. Watafaulu katika uongozi wao ikiwa watasaidia wanajumuiya waweze
kujiuliza maswali yaliyo sahihi na wakijitahidi kukumbuka kuwa majibu ya maswali sahihi
hupatikana katika kujiuliza maswali hayo kwa pamoja. Tunawapongeza na kuwatakia Baraka
za Mwenyezi Mungu katika utume wao huu mpya.
Pd. Felix Mushobozi, C.PP.S.,
Katibu Mkuu wa Shirika.