2010-04-30 15:25:48

Kardinali Paul Augustin Mayer afariki dunia


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita amewatumia Wabenediktini salam za rambi rambi kutokana na kifo cha Kardinali Paul Augustin Mayer, kilichotokea ijumaa tarehe 30 Aprili, 2010, mjini Roma. Baba Mtakatifu anasema, kifo cha Kardinali Meyer kinaacha chapa ya kudumu katika utume wake kwa Kanisa, kazi ambayo aliifanya kwa majitoleo na unyenyekevu mkubwa mintarafu wito wa maisha yake ya kimonaki.

Kardinali Mayer alikuwa ni mchungaji aliyejitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya uenezaji wa Injili, alikuwa mwaminifu kwa Kristo na Kanisa. Alijitahidi kuboresha Liturjia na majiundo ya wale waliokuwa kwenye vyuo vikuu, lakini jambo la msingi zaidi ni huduma aliyoitoa wakati wa uongozi wake kwenye Kamati ya Maandalizi ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na kwenye Mabaraza mbali mbali ya Kipapa mjini Vatican.

Baba Mtakatifu anamwombea Marehemu Kardinali Mayer ili aweze kupata pumziko la milele miongoni mwa watakatifu. Baba Mtakatifu anawahakikishia ukaribu wake kwa njia ya sala, wote walioguswa na msiba huu mzito.

Ibada ya Misa ya Mazishi inatarajiwa kufanyika jumatatu tarehe 3 Mei, 2010, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kuongozwa na Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali. Baada ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, anatarajiwa kutoa mahubiri.

Kardinali Mayer alizaliwa kunako tarehe 23 Mei, 1911, Jamhuri ya watu wa Ujerumani. Mwaka 1931 aliweka nadhiri za kitawa katika Shirika la Wabenediktini. Tarehe 25 Agosti, 1935 alipewa Daraja Takatifu la Upadre. Kwa miaka zaidi ya ishirini na saba alijitoa mhanga kwa ajili ya kufundisha pamoja na kushika nyadhifa mbali mbali za uongozi. Ni muasisi wa Taasisi ya Kipapa ya Liturjia, ambayo imekuwa ni kitovu cha majiundo ya Majaalimu ya Kanisa katika Liturjia na Seminari, sehemu mbali mbali za dunia.

Hayati Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa pili alimteua kuwa Kardinali kunako tarehe 25 Mei, 1985. Kwa kifo cha Kardinali Mayer, idadi ya Makardinali imebaki kuwa ni 180, kati yao 108 wanahaki ya kupiga na kupigiwa kura wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kati yao 72 ni watazamaji tu.







All the contents on this site are copyrighted ©.