Waathirika wa Ukimwi Uganda ni kielelezo cha upendo wa mshikamano, watu wapya katika
imani!
Askofu Beatus Kinyaiya wa Jimbo la Mbulu, Tanzania anasema, uharibifu wa mazingira
unatishia mistu na uoto wa asili Barani Afrika na matokeo yake yake ni madhara yanayoendelea
kujitokeza sehemu mbali mbali ya Bara la Afrika. Ukame wa kutisha, mafuriko, mmomonyoko
wa udongo na athari zake kiasi cha kuwafanya watu kuwa ni wahanga wa mabadiliko ya
tabianchi. Binadamu ajifunze kulinda na kutunza mazingira kwa ajili ya kizazi hiki
na kile kijacho.
Watalii kutoka sehemu mbali mbali za dunia wamechangia katika
shughuli za kiuchumi Barani Afrika, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba, Kanisa
Barani Afrika alikutumia fursa hii kama sehemu ya Uinjilishaji kwa kuhakikisha kwamba,
watalii wanasaidia katika mahitaji yao ya maisha ya kiroho.
Ni jukumu la Mababa
wa Sinodi kuangalia uwezekano wa kuteuwa mapadre watakaowasaidia watalii katika mahitaji
yao ya maisha ya kiroho wanapotembelea Bara la Afrika.
Sr. Mary Anne Felicitas
Katiti, Mama mkuu wa Kanda wa Shirika la Dada Wadogo wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi
ya Asili, amewasihi Mababa wa Sinodi kuendelea kuwathamini wanawake katika huduma
kwa Kanisa na jamii wanaposhiriki katika azma ya Uinjilishaji wa kina.
Ni
watu wanaoteseka na kubeba magumu ya maisha ya kifamilia na kwa kiais kikubwa wao
wamekuwa ni wahanga wa nyanyaso za kijinsia. Wanawataka wanaume kuondokana na mfumo
dume unaowakandamiza na kuwanyima haki zao msingi.
Yesu Kristo alileta mapinduzi
ya kweli katika kumkomboa mwanamke, kiasi cha kuwashirikisha katika utume wake, wanawake
wakawa wa kwanza kupokea Habari Njema ya ufufuko wa Kristo. Wanawake wanasubiri haki
na heshima kutoka ndani ya Kanisa na Jamii kwa ujumla.
Mama Rose Busingye,
m wanzilishi na Rais wa Meeting Point International, kutoka Kampala, Uganda anasema
imani haina budi kupenya katika maisha ya mwanadamu, ili iweze kumwilishwa na kutolewa
ushuhuda wa maisha kwa ajili ya mafao ya wengi pamoja na kukoleza furaha, haki na
amani.
Ili kufanikisha mchakato wa ujenzi wa upatanisho, haki na amani, mwanadamu
na mahitaji yake msingi hana budi kupewa kipaumbele, kwa kuthamini zawadi ya maisha
na kuenzi utu na heshima ya mwanadamu. Huu ndio msaada mkubwa unaoweza kutolewa na
Mama Kanisa Barani Afrika.
Imani anasema Mama Rose Busingye ambaye amekuwa
mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi kwa kuonesha mshikamano
na waathirika inaweza kumletea mtu mabadiliko. Huu ndio muujiza wa imani kwa waathirika
wa Ukimwi nchini Uganda ambao wanaendelea kufanya kazi kwa ajili ya kujipatia riziki
yao ya kila siku, licha ya magumu wanayokabiliana nayo.
Ni watu wanaoendelea
kuonesha moyo wa mshikamano na watu wengine wanaoathirika kwa majanga asilia sehemu
mbali mbali za dunia. Wanatambua kwamba, moyo wa mwanadamu ni wa kimataifa hauna rangi
wala kabila.