2009-09-23 10:57:05

B16: Mt. Anselmi awe ni mfano wa kuigwa katika tafakari ya mafumbo ya imani ya Kikristo, ili kujenga upendo kwa Mungu na jirani


Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, siku ya jumatano asubuhi, tarehe 23 Septemba, 2009 alirejea tena mjini Vatican akitokea Ikulu ndogo ya Castel Gandolfo, ili kuwamegea katekesi mahujaji na wageni waliofika mjini Vatican.

Mtakatifu Anselmi, mwana mahiri wa Kanisa, aliyeishi kunako karne ya kumi na moja, ndiye aliyekuwa kiini cha kateksi ya Baba Mtakatifu siku ya jumatano. Ni mtu aliyepokea elimu ya kimonaki kwenye mji wake wa Aosta, Kaskazini mwa Italia, alikozaliwa na baadaye kujiunga na Monasteri ya wa Wabenediktini huko Bec, Normandy.

Mtakatifu Anselmi alipata malezi yake ya kimonaki chini ya mkuu wake Lanfranc wa Pavia, akajitoa bila ya kujibakiza kwa sala na masomo na hatimaye akateuliwa kuwa ni mkuu wa Abbasia ya Bec na baadaye aliteuliwa kuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cantebury, Uingereza.

Akiwa nchini humo, alijikuta akikabiliana na mabadiliko makubwa ya maisha ya kikristo yaliyotokana na uvamizi wa watu kutoka Kaskazini pamoja na jitihada za Kanisa kujitafutia uhuru wake kutoka kwenye makucha ya wanasiasa, hali iliyompelekea kutupwa gerezani kwa kipindi cha miaka mitatu.

Mtakatifu Anselmi alikuwa ni ni kiongozi mahiri katika maisha ya kiroho, mwalimu aliyetukuka, mwandishi mashuhuri na mwanataalilimungu makini. Ni mtu aliyependa kuifahamu imani na kweli za kimungu ambazo moyo wake ulikuwa tayari umebahatika kuziamini na kuzipenda.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuiga mfano wa maisha ya Mtakatifu Anselmi, katika kufanya tafakari ya kina juu ya Mafumbo ya imani ya Kikristo, ili kujenga upendo mkubwa zaidi kwa Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita kwa mara nyingine tena amewaomba waamini kumsindikiza kwa njia ya sala na sadaka yao, wakati wa ziara yake ya kichungaji Jamhuri ya Watu wa Czech, ili iweze kuzaa matunda ajaa ya maisha ya kiroho.

Mtakatifu Anselmi awe ni mfano hai na wa kuigwa katika jitihada za mwamini kudumisha umoja na Kristo katika kifungu cha upendo kwa Mungu na jirani. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu ameungana na familia za watu walioathirika kutokana na maporomoko ya machimbo ya madini nchini Poland. Anawaombea marehemu wote waliopoteza maisha yao, ili wapate pumziko la milele na wagonjwa wapate nafuu na hatimaye kupona haraka.

Baba Mtakatifu amewataka wanajeshi waliohudhuria kwenye kateksi yake mjini Vatican, kuendelea kutolea ushuhuda tunu msingi za kiutu na kikristo, ili kujenga jamii inayosimikwa katika uhuru na mshikamano wa kweli.







All the contents on this site are copyrighted ©.