2009-07-07 08:38:18

Ndoto ya kufikia Malengo ya Mendeleo ya Millenia yazidi kuyoyoma


Hati ya tatu ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita Caritas In Veritate, Upendo katika Ukweli, inachambua kwa kina masuala mbali mbali ya kijamii mintarafu Mwanga wa Injili na ukweli katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo ya Millenia, ifikapo mwaka 2015, jambo ambalo kadiri ya wachunguzi wa masuala ya kijamii, ni ndoto kuweza kufikiwa kutokana na mwenendo wa hali ya uchumi wa kimataifa kwa sasa.

Social Watch, Shirika la Lisilo la Kiserikali linalojihusisha na masuala ya kijamii linatabiri kwamba, pengine Malengoo ya Maendeleo ya Millenia kwa Afrika yanaweza kufikiwa, hapo mwaka elfu mbili na ishirini, na Asia ya Kati inaweza kufikia Malengo hayo ifikapo mwaka elfu mbili na arobaini. Wimbi la umaskini linazidi kuongezeka maradufu duniani, tofauti kabisa na takwimu zilizokuwa zimetolewa na Benki ya Dunia kwa mwaka elfu mbili na nane.

Hali ya maisha kijamii kwa watu wanaoishi Kusini mwa Jangwa la Sahara inazidi kudorola ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita. Haya ni matokeo ya mfumuko wa bei ya mazao ya chakula iliyojitokeza mwaka 2006, kupanda kwa gharama ya nishati pamoja na kuchechemea kwa uchumi wa kimataifa. Yote haya yanapelekea kutofikiwa kwa Malengo ya Maendeleo ya Millenia, kama ilivyokuwa imepangwa na Umoja wa Mataifa kwa Mwaka 2015.

Social Watch, inazitaka nchi tajiri kufanya mabadiliko makubwa katika kukabiliana na mtikisiko wa kiuchumi, kusaidia kuboresha hali ya usalama wa chakula kwa nchi changa, matumizi ya nishati salama na rafiki kwa mazingira na udhibiti wa uchafuzi wa mazingira duniani. Yote haya yajengeke katika msingi wa haki na ushirikiano wa kimataifa, kwa lengo la kuboresha hali ya uchumi wa kimataifa na madhara yake kwa nchi zinazoendelea duniani.

Umoja wa Mataifa ulikuwa umejiwekea Malengo ya Maendeleo ya Millenia ifikapo Mwaka 2015, ili kutokomeza balaa la njaa, umaskini, utoaji wa elimu kwa wote, kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wenye umri mdogo, kukuza usawa wa kijinsia, kuboresha mazingira, kupambana na ukimwi pamoja na malaria, magonjwa ambayo yamekuwa ni sababu ya vifo vya watu wengi katika Nchi Zinazoendelea.

Uchafuzi wa mazingira, ukame wa kutisha, ongezeko la Jangwa Kusini mwa Sahara na kwamba, kuna watu zaidi ya millioni mia moja na thelathini na tano, katika kipindi cha miaka kumi kuanzia sasa hawatakuwa na makazi. Watu zaidi ya Billioni moja nukta mbili hawapati huduma ya maji safi na salama. Na kwamba, kuna watu Billioni mbili nukta nne, hawapati huduma ya afya ya msingi duniani.

Nchi wahisani wamepunguza kwa kiasi kikubwa mchango wao kwa ajili ya kugharimia Malengo ya Maendeleo ya Millennia. Wachunguzi wa masuala ya kiuchumi wanasema, kuna haja pia kwa wahisani kuratibu na kuhakikisha kwamba, misaada inayotolewa kwa nchi zinazoendelea inawafikia walengwa, vinginevyo, inaweza kuishia kwenye mikono ya mafisadi na wahujumu uchumi.

Hati ya tatu ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita inayaangalia masuala ya kijamii na kujitahidi kutoa mwelekeo wa matumaini, ili dunia iendelee kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.







All the contents on this site are copyrighted ©.