Bajeti ya Uganda kuwa ya kiasi: vipaumbele: miundombinu na nishati
Waziri wa fedha wa Uganda Sydda Bbumba amesema, Serikali ya Uganda katika bajeti
yake kwa mwaka 2009/2010 inatarajia kuwekeza zaidi kwenye miundo mbinu na nishati,
kukiwa na ongezeko kidogo sana la bajeti.
Uganda kwa miaka mingi imekuwa ikiongoza
kwa sekta ya utalii na uzalishaji wa Kahawa, lakini kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita
huduma na uzalishaji viwanadani umeendelea kuongezeka, lakini sekta ya kilimo ambayo
inatoa fursa ya ajira kwa asilimia sabini ya wananchi wa Uganda imedumaa, hasa baada
ya wawekezaji kutoka nchi za nje kugundua uwepo wa nishati ya mafuta nchini Uganda,
katika mipaka yake na Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Congo.
Serikali ya
Uganda inatarajiwa kutumia kiasi cha shilingi Trillioni sita nukta mbili saba, sawa
na Dolla za Kimarekani Billioni mbili nukta tisa nne. Ufinyu wa bajeti hii unatokana
pia na mtikisiko wa uchumi kimataifa pamoja na hali ngumu ya kiuchumi inayozikabilia
nchi nyingi wahisani.
Wachunguzi wa mambo ya kiuchumi wanasema, Serikali ya
Uganda inapaswa kudhibiti mfumuko wa bei ya bidhaa na huduma. Kilimo kinatarajiwa
pia kupewa msukumo wa pekee katika bajeti ya Uganda inayotangazwa siku ya alhamisi
tarehe 11 Juni, 2009.