Utamaduni wa upendo na mshikamano kuwafaidisha Watoto wa Kijiji cha Matumaini Dodoma
na Hospitali ya Mt. Gaspar, Itigi
zaidi ya Euro hamsini na tatu elfu zimekusanywa na wanachama wa Chama cha Ushirika
cha Legnaria, kilichoko mjini Firenze, Kaskazini mwa Italia, ili kuonesha mshikamano
wa upendo na wananchi wa Tanzania katika utoaji wa huduma kwa wagonjwa na watoto walioathirika
kwa virusi vya Ukimwi.
Kitivo cha Kilimo cha Chuo Kikuu cha Firenze kwa kushirikiana
na wadau mbali mbali wamekusanya fedha zitakazotumika kuendeshea shughuli za huduma
ya elimu, tiba, chakula na malazi kwa watoto zaidi ya mia moja hamsini wanaoishi na
virusi vya ukimwi na kuhudumiwa kwenye Kijiji cha Matumaini, kinachomilikiwa na kuendeshwa
na Masisita Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu.
Hospitali ya Mtakatifu Gaspar iliyoko
Itigi, mkoani Singida, inamilikiwa na kuendeshwa na Wamissionari wa Damu Takatifu
ya Yesu, na imekuwa mstari wa mbele katika kuokoa maisha ya watu kwa tiba na kinga
ya magonjwa, hasa kwa kutoa kipaumbele kwa ajili ya huduma ya watoto. Hospitali ya
Mtakatifu Gaspar, Itigi kwa sasa ina jumla ya vitanda mia nne kwa wagonjwa wanaolazwa,
kati ya vitanda hivi, watoto wametengewa vitanda mia tatu.
Akizungumzia kuhusu
lengo la mradi huu, Professa David Bocciolini, Rais wa Chama cha Ushirika cha Wakulima
wa Legnaia wakishirikiana na Kitivo cha Kilimo cha Chuo Kikuu cha Firenze, Italia,
wanataka kuanza kufanya majaribio ya kilimo cha mpunga katika nchi kavu kwa kutumia
maji kidogo yanayopatikana katika maeneo ya Sindiga, ambayo hayana uhakika wa mvua
na mara kwa mara yanakabiliwa na balaa la njaa.
Pili ni kufanya uchunguzi
wa magonjwa yanayoshambulia mazao, ili kuwaongezea tija na mapato wakulima, ili hatimaye
waweze kuwa na uhakika wa usalama wa chakula na pato kutokana na shughuli za uzalishaji
katika sekta ya kilimo.
Tatu, ni kusaidia kuwaandaa watalaamu watakaoendeleza
sekta ya kilimo na ufugaji, ili kuongeza uzalishaji wa maziwa kwa ngo'mbe wanaofugwa
kwenye Kijiji cha Matumaini kwa ajili ya matumizi ya watoto walioathirika kwa ugonjwa
wa Ukimwi pamoja na wale wanaofugwa Hospitali ya Mtakatifu Gaspar, Itigi. Hii ni kati
ya Hospitali za kisasa zilizoko Kanda ya Kati, inayotoa huduma zake hadi vijijini
kwa njia ya Zahanati zilizoko chini ya usimamizi wake.
Akizungumza kwenye hafla
ya kuchangisha fedha kwa ajili ya Mradi wa Tanzania, Padre Sebastiano Benedettini,
C.PP.S, aliwashukuru sana waamini na watu wenye mapenzi mema kutoka Jimbo la Firenze,
ambao kwa takribani miaka arobaini, wamekuwa mstari wa mbele katika ujenzi wa utamaduni
wa upendo na mshikamano, jambo ambalo limewawezesha Wamissionari wa Damu Takatifu
ya Yesu kuanzisha Hospitali na huduma ya maji. Wao ndio waliokuwa wadau wa kwanza
wa jitihada hizi za kimissionari chini ya Uongozi thabiti wa Padre Mario Dariozzi,
C.PP.S, utamaduni ambao wameuendeleza hadi sasa.
Baadhi ya waamini waliokuwepo
kwenye hafla hiyo walisema kwamba, Kwaresima ya mwaka 1976, ilifungua moyo wa ushirikiano
na upendo na watu wa Tanzania, katika jitihada zao za kupambana na umaskini, ujinga
na maradhi, kwa kuchangia fedha zilizotumika kutengenezea mashine za kusukuma maji,
mradi ambao hadi sasa unajulikana kama C.PP.S Mission Water Project, tegemeo la huduma
za maji safi na salama kwa wananchi wa mikoa ya Kanda ya Kati Tanzania.