Matumizi haramu ya madawa ya kulevya yana athari zake si tu kwa mtumiaji bali hata
kwa familia na jamii kwa ujumla. Padre Flavian Kassala Matindi kutoka Jimbo Katoliki
la Geita, Tanzania anapembua kwa kina juu ya madhara ya matumizi haramu ya madawa
ya kulevya.
Wapendwa vijana,
tunaendela na makala yetu juu ya madawa ya kulevya na madhara yake kwa jamii na
kwa namna ya pekee kwa vijana. Baada ya kuwa tumeangalia kwa undani maana halisi ya
madawa ya kulevya, hatuna budi leo kuangalia ni nini matokeo ya utumiaji wa madawa
haya.
Kwa ujumla hakuna hata faida moja aipatayo mtu kwa kutumia madawa haya.
Hali yoyote ya utulivu na kuridhika inayotokea baada ya kutumia madawa haya ni ya
mpito tu na kwa kweli ni mwanzo wa safari kuelekea kuharibikia maisha. Mtumiaji yeyote
wa madawa ya kulevya hujisikia faraja inayotokana na kusahau mazingira na hasa matatizo
yanayomzunguka kwa wakati huo. Hali hii ambayo hudumu kwa muda mfupi tu hufuatiwa
na maumivu na hali ya usingizi ambayo humsambabishia mtumiaji mfadhaiko mkubwa wa
kimaisha. Ni hali hii ya mfadhaiko inayomsukuma mtumiaji kutafuta tena dozi nyingine
ya madawa hayo.
Wataalamu wanaeleza kuwa hali ya utulivu na ugenishwaji wa
matatizo binafsi si matunda ya madawa kana kwamba ni kitu kinachosaidia kuachana na
matatizo yanayotuzunguka. Kwa kweli kinachotokea ni kwamba madawa ya kulevya baada
ya kuwa yametumiwa na mtu yeyote hupunguza uwezo wa kupumua, hushusha mapigo ya moyo
na msukumo wa damu. Hali hizi kwa kweli ni safari ya kuelekea katika kuzimia, kuingia
katika koma, mapafu kushindwa kufanya kazi yake kwa ufasaha na mwisho wake ni kifo.
Madhara haya yaletwayo na madawa ya kulevya yanatokana na sumu mbalimbali
zilizochanganya katika kutengeneza madawa haya. Baadhi ya kemikali zinazotumika katika
kuchanganya madawa haya ni pamoja na petroli na maji ya betri za magari na pikipiki
yaani sulphuric acid.
Madawa ya kulevya, iwe yale ya kiasili kama bangi au
yale yatengenezwayo kimaabala kama vile heroin, husababisha mtu kuwa tegemevu. Mtumiaji
wa madawa ya kulevya hufikia mahali ambapo hawezi kufanya jambo lolote bila ya kutumia
madawa hayo. Ukizingatia pia bei kubwa ya madawa haya, matokeo ya kwanza kwa mtumiaji
ni umaskini. Hali hii ya kuwa tegemevu na umaskini unaotokana na kutumia kila kitu
ili kupata madawa haya hufuatiwa na tabia ya wizi, utekaji nyara na tabia zingine
zozote haramu ambazo huweza kumpatia mtumiaji vijisenti walau kidogo tu kwa ajili
ya kununua madawa ya kulevya.
Pamoja na uharifu, utumiaji wa madawa ya kulevya
una uhusiano makubwa sana na maambukizo ya ukimwi. Kwanza kabisa ni kutokana na ukweli
kwamba watumiaji wa madawa haya huchangia sindano ambazo wanatumia kwa kujidunga madawa
haya. Hali hii husababisha maambukizi ya ukimwi kwa kasi zaida iwapo katika kundi
kuna mtu aliyeathirika tayari. Matumizi ya madawa ya kulevya huathiri utashi wa mtu.
Na hivyo mtu hutenda mambo yake yote kulingana na hisia zinavyomtuma. Kwa hali hiyo
matumizi ya madawa ya kulevya yamekuwa yakihusishwa na matukio mengi ya ubakaji ambao
matokeo yake kwa kiasi kikubwa ni kuambukizwa au kuambukiza ukimwi.
Mtume Paulo
anatualika kwa upendo na kutukumbusha, “Je hamjui miili yenu ni viungo vya Kristo?”
Ni swali linalotupatia changamoto kutafakari kwa kina madhara ya makusudi ambayo yanahatarisha
muungano wetu na jamii, na Mungu. Madawa ya kulevya ni sababu kubwa inayochangia mtengano
huo hasa kwa vijana katika kizazi chetu hiki. Anandelea kutukumbusha Mtume Paulo “Au
hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu?” Zaidi sana wapendwa vijana
mkumbuke kuwa ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi,
mtukuzeni Mungu katika miili yenu.” (1 Wakor. 6:15 - 20).