2008-10-25 10:24:36

UJUMBE WA MABABA WA SINODI KWA WATU WA MUNGU


Sinodi ya Maaskofu iliyokuwa inajadili juu ya Neno la Mungu katika maisha na utume wa Kanisa, imefungwa rasmi siku ya jumapili kwa Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baada ya kikao, Mababa wa Sinodi wameandika ujumbe kwa ajili ya watu wa Mungu unaogusa mambo msingi waliyotafakari na hatimaye kutolea ushauri kuhusu Neno la Mungu kama kiini cha utume wao wakati wote wa Sinodi.
Kimsingi ujumbe huu unawalenga viongozi wa Kanisa waliyopewa dhamana na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanawamegea waamini Neno la Mungu. Ujumbe huu unatumwa kwa makatekista ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia wakatekumeni kulifahamu Neno la Mungu pamoja na watu wengine wote ambao wamejitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwasaidia waamini kusikiliza na kulisoma Neno la Mungu. Mababa wa Sinodi wanazama ndani zaidi katika ujumbe wao, ili kulisaidia Taifa la Mungu, kulipenda na hatimaye, kujitajirisha na Neno la Mungu. Ili kuifikia azma hii, mambo makuu manne yametiliwa mkazo na Mababa wa Sinodi katika ujumbe wao kwa taifa la Mungu kwamba:
Mosi, Neno la Mungu ni sauti ya Mungu iliyojidhihirisha tangu mwanzo wakati wa kazi ya uumbaji, kwa kuvunja kimya na utupu uliokuwepo na hapo Mwenyezi Mungu akaonesha maajabu yake kwa kuumba ulimwengu. Hii ni sauti ya Mungu inayopenya katika historia ya maisha ya mwanadamu aliyejeruhiwa kwa uwepo wa dhambi pamoja na kukata tamaa kutokana na taabu pamoja na kifo. Mwenyezi Mungu anaendelea bado kufanya hija na Taifa lake kwa njia ya Neema, Agano lake la Milele na kwa njia ya ukombozi. Hii ndiyo sauti inayoingia katika Maandiko Matakatifu, Inayosomwa Kanisani, kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu, anayetoa mwanga wa ukweli kwa Neno la Mungu na wachungaji wake.

Pili, huyu ndiye Neno aliyefanyika mwili, kama anavyoandika Mtakatifu Yohane, nasi tumebahatika kuuona uso wake, Yaani Yesu Kristo, Mwana wa Mungu wa milele. Tumeuona ubinadamu wake, uliosongwa na mauti, akafungwa katika historia ya nyakati, kati ya watu na nchi inayoweza kutambulika. Yesu alijitahidi kuuishi ubinadamu wake katika ukamilifu, isipokuwa hakuwa na dhambi hadi kifo cha Msalaba, lakini akafufuka kutoka katika wafu, kama ilivyoandikwa na sasa anaishi milele.

Anakamilisha uhusiano kati ya mwamini na Neno la Mungu. Anamkirimia mwamini uelewa na Umoja unaofumbatwa katika Maandiko Matakatifu, kwa maana hii, Ukristo ni dini inayopata msingi wa uhai wake kwa Yesu Kristo, anayewafunulia waamini Mwenyezi Mungu. Anawasaidia waamini kulifahamu Neno la Mungu katika maneno ya wanadamu, wakijitahidi kujifunza kwa kutumia njia na maneno yao, lakini daima wakitunza ndani yake ule mwanga wa ukweli wa Kimungu, unaowawezesha waamini kuishi na kutafakari pamoja na Roho Mtakatifu.

Tatu, Mababa wa Sinodi wanasema, Roho Mtakatifu anawaongoza waamini katika hija ya maisha yao katika Nyumba ya Neno la Mungu, ambayo ni Kanisa, kama anavyobainisha Mwinjili Luka, katika kitabu chake cha Matendo ya Mitume 2:42. Ni mahali ambapo waamini wanajichotea Mafundisho ya Neno la Mungu, kwa kusoma na kujitahidi kuielewa Biblia kwa wote, katika katekesi, mahubiri na utangazaji wa Neno hili unaogusa akili na moyo wa mwanadamu. Ndani ya nyumba hii, waamini wanashiriki katika Kuumega Mkate kwa njia ya Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kama ilivyojidhihirisha wakati Yesu alipokutana na wanafunzi wa Emmaus.

Waamini wanaalikwa kujitajirisha kwa Liturjia ya chakula cha Neno la Mungu na Mwili wa Kristo, katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Mababa wa Sinodi wanakumbusha kwamba, hii ni nyumba ya sala inayopambwa kwa Zaburi, Tenzi na Nyimbo zinazojichotea utajiri wake kutoka katika Neno la Mungu. Ni nyumba ya Sala ya Kanisa, inayoliwezesha Kanisa kumwimbia Mungu sifa kila siku na nyakati zote za Mwaka wa Kanisa. Kuna Sala ya Neno la Mungu, inayojulikana kwa lugha ya Kitaalamu: Lectio Divina, Njia Sala katika usomaji wa Neno la Mungu, kulitafakari kama njia ya kukutana na Yesu aliye hai. Mwishowe, kuna umoja wa kidugu, kwani kwa wakristo, haitoshi kusikiliza Neno la Mungu tu, bali wanapaswa pia kulimwilisha katika maisha yao, kwa njia ya matendo ya mapendo. Kwenye Nyumba ya Neno la Mungu, waamini wanakutana na ndugu zao kutoka Makanisa na Madhehebu mengine ya Kikristo, hata katika utengano wao, lakini bado wanaishi katika Umoja wa Kanisa, kwa njia ya kuabudu na kulipenda Neno la Mungu.
Sehemu ya Nne katika Ramani hii ya maisha ya kiroho, Mababa wa Sinodi wanawakumbusha waamini kwamba, wanatumwa kwenda kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho yote ya dunia, kwa kuwafundisha kushika yote aliyoamuru Kristo, yale ambayo wameyasikia katika kificho, wayatangaze juu ya pawa za nyumba. Neno la Mungu halina budi kuhakikisha kwamba, linaingia hata kwenye njia za mawasiliano ya Kisasa: Kwenye Familia, ili wazazi na watoto wao waweze kuisoma, kuisali na hatimaye iwe ni taa katika hija ya maisha yao.

Mababa wa Sinodi wanatoa changamoto kwamba, umefika wakati sasa Biblia kujipenyeza kwenye shule na taasisi za elimu, kwani huko ndiko, kwa miaka mingi Neno la Mungu limekuwa ni kiini rejea kwa Sanaa, Machapisho, Muziki, Fikira na Maadili. Uwezo na utajiri wa Neno la Mungu katika matumizi ya lugha ya picha, ushairi na simulizi, unakoleza utamu wa imani na utamaduni, katika ulimwengu ambao kwa kiasi kikubwa unapambwa na ubaya pamoja na upweke.
Mababa wa Sinodi katika ujumbe wao, wanasema, Biblia pia inaonesha taabu zinazoibuka katika uso wa dunia, hiki ni kilio cha watu wanaodhulumiwa, wanaolalamika kuhusu hali yao ya maisha. Kilele chake ni pale juu ya Msalaba, Kristo mwenyewe, aliyebaki peke yake baada ya wafuasi wake wa karibu kutimua mbio, aliweza kuyamimina maisha yake kwa njia ya mateso na kifo. Lakini kwa vile Yesu ni Mwana wa Mungu, giza la dhambi na mauti linashindwa kwa Mwanga wa Pasaka, kwa njia ya matumaini na utukufu. Mababa wanawakumbusha waamini kwamba, katika hija ya maisha yao hapa duniani, ndugu wa kutoka Makanisa mengine pamoja na madehehbu ya kikristo wanafanya hija hii ya maisha, hata katika hali hii ya utengano, wanaendelea kuonesha umoja wao kwa kuliabudu na kulipenda Neno la Mungu. Katika hija hii, wakristo wanakutana na waamini wa dini mbali mbali duniani wanasikiliza kwa makini na kumwilisha ujumbe wa Vitabu vyao vitukufu, ambao wakiungana pamoja na wakristo, wanapania kujenga ulimwengu unaosimikwa katika Amani na Mwanga, kwani Mwenyezi Mungu anapenda watu wote waokoke na kuufahamu ukweli.
Mababa wa Sinodi wanawaalika waamini kulinda Biblia katika nyumba zao, kuisoma, kujifunza kwa dhati kabisa pamoja na kujitahidi kuuelewa ujumbe wa Neno la Mungu katika maisha, ili uweze kuwasaidia kugeuka na kuwa ni watu wa sala wanaolitolea ushuhuda, wanaolisikiliza kwa upendo na imani katika liturjia. Mababa wanawaomba waamini kujenga ukimya, ili Neno la Mungu liweze kupenya na kufanya makao yake katika maisha ya waamini. Mwangi wa Neno la Mungu usikike katika maisha ya waamini wanapoianza siku yao na wakati wa jioni, wanapokunja jamvi la maisha yao ya siku.
Mababa wa Sinodi wanahitimisha ujumbe wao kwa Familia ya Mungu kwa maneno ya Mtakatifu Paulo mtume na Mwalimu wa Mataifa kwa kuwaaga na kusema kwamba: basi sasa ninawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa Neno la neema yake. Mababa wa Sinodi wanawaaminisha waamini walioenea sehemu mbali mbali za dunia juu ya Neno la Mungu kama hukumu, lakini zaidi kama Neema, inayoweza kufananishwa na upanga unaokata kuwili, lakini ni tamu kama sega la asali. Lina nguvu na utukufu, linalowaongoza katika njia ya Historia pamoja na Yesu, wanaompenda kama wanavyofanya wao.







All the contents on this site are copyrighted ©.